Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM),Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa leo Jumanne, Oktoba 28, 2025, kuhitimisha rasmi kampeni zake za Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kwa kufanya mkutano wa hadhara katika Viwanja vya CCM Kirumba, jijini Mwanza.

Samia, mwenye umri wa miaka 65, anaingia katika kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu wa kesho Jumatano akiwa na historia ya kipekee kama mwanamke wa kwanza kuidhinishwa na CCM kugombea nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hapo awali, aliweka historia nyingine kwa kuwa Makamu wa Rais na baadaye Rais wa kwanza mwanamke katika historia ya taifa hilo.
Kwa mujibu wa taarifa za chama hicho, katika kipindi cha siku 60 za kampeni, Samia amefanya mikutano ya hadhara 114 katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Katika Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2025–2030, Samia ameahidi kuendeleza na kuimarisha mageuzi ya kiuchumi kwa kuhimiza uchumi wa kisasa, jumuishi na shindani; kuongeza fursa za ajira kwa vijana; kupunguza umaskini; na kuboresha ustawi wa wananchi. Pia ameahidi kudumisha demokrasia na utawala bora, ikiwemo kuanzisha mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya.
Tangu aingie madarakani mwaka 2021, Samia amekuwa akisisitiza uwepo wa maridhiano akisisitiza falsafa yake ya “4R” — Reconciliation, Resilience, Reforms and Rebuilding ambayo imetumika kuwakutanisha pamoja wapinzani wake. Hata hivyo falsafa hiyo kwa sasa inaonekana kwenda kinyume na mitazamo ya wengi kutokana na shutuma dhidi yake juu ya ukiukwaji wa haki, ukandamizaji wa demokrasia na hata kuwakandamiza wapinzani wake kisiasa.