Uchaguzi wa Tanzania wa 2025 umegubikwa na hofu, ukandamizaji wa kisiasa, na wasiwasi wa kimataifa kuhusu mustakabali wa demokrasia nchini, huku Rais Samia Suluhu Hassan akielekea kushinda bila upinzani wa kweli.

Tanzania inapiga kura leo, Oktoba 29, 2025, katika uchaguzi mkuu unaoonekana kumwendea Rais Samia Suluhu Hassan, anayewania muhula wa pili kupitia CCM. Uchaguzi huu umechochea mjadala mkali kuhusu uhuru wa kisiasa na haki za binadamu, hasa baada ya kuenguliwa kwa wagombea wakuu wa upinzani.
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA, ilikosa nafasi ya kushiriki kikamilifu baada ya mgombea wake Tundu Lissu kukamatwa kwa tuhuma za uhaini, hali iliyozuia chama kuwasilisha mgombea mbadala. Lissu ambaye ashawahi kuwa mgombea urais mwaka 2020, anashtakiwa kwa kutoa hotuba iliyodaiwa kuchochea ghasia dhidi ya uchaguzi.

Luhaga Mpina wa ACT Wazalendo pia alizuiwa kugombea kwa mara ya pili, na hivyo kuacha nafasi ya urais ikigombewa na wagombea wasiojulikana sana kitaifa. Mashirika ya kutetea haki za binadamu, yakiwemo Human Rights Watch, Amnesty International, na LHRC, yameonya kuwa uchaguzi huu unafanyika katika mazingira ya hofu, ukandamizaji wa vyombo vya habari, na kukosekana kwa uhuru wa kiraia.

Amnesty International ilieleza kuwa serikali ya Rais Samia imeendeleza mbinu za ukandamizaji zilizokuwepo chini ya mtangulizi wake, John Magufuli, ikiwemo kutoweka kwa wakosoaji wa serikali na mauaji ya kiholela mwaka 2024. Serikali ya Tanzania imekanusha ripoti hizo, ikidai kuwa ni za upotoshaji na hazikuwapa nafasi ya kujibu kabla ya kuchapishwa.
Kwa sasa, hali ya taharuki imetanda nchini, huku wapiga kura wakielekea vituoni bila uhakika wa mwelekeo wa kisiasa wa taifa lao. Watazamaji wa ndani na nje wanatazama kwa makini ikiwa uchaguzi huu utakuwa hatua ya kuimarisha utawala wa kiimla au mwanzo wa mabadiliko ya kidemokrasia.