Mwigizaji Will Smith alivamia jukwaa la tuzo za Oscar na kumzaba kofi mcheshi Chris Rock usoni kwa kumtania mke wake, katika muda mfupi kwenye tamasha la Jumapili ambalo lilisambaa mitandaoni mara moja — na kuwaacha waliohudhuria na watazamaji wakishangaa.
Rock, akiwasilisha hotuba fupi alipokuwa akitoa tuzo bora katika kitengo cha ‘Best Documentary”, alifanya mzaha akilinganisha nywele za Jada Pinkett Smith alizonyoa na mwonekano wa Demi Moore katika filamu ‘GI Jane’ na akapendekeza aonekane katika mwendelezo wa filamu hiyo.
Katika tukio ambalo liliwaacha wengi vinywa wazi katika Ukumbi wa Kuigiza wa Dolby, Smith alimuendea Rock na kumpiga kofi, kabla ya kurudi kwenye kiti chake huku akimtusi Chris Rock.
“Ondoa jina la mke wangu kinywani mwako,” alifoka Smith.
Idara ya Polisi ya Los Angeles ilisema “inafahamu” tukio hilo “lililohusisha mtu mmoja kumpiga mwenzake kofi,” lakini kwamba “mtu aliyepigwa kofi amekataa kuwasilisha ripoti kwa polisi.”
“Ikiwa mhusika atataka kuwasilisha ripoti kwa polisi baadaye, LAPD itapatikana ili kukamilisha ripoti ya uchunguzi,” ilisoma taarifa ya idara iliyopatikana na AFP.
Baada ya tamasha kumalizika, Academy Awards iliandika kwenye Twitter kwamba “haikubaliani na vurugu za aina yoyote,” bila kurejelea tukio hilo moja kwa moja.
“Usiku wa leo tunafuraha kusherehekea washindi wetu wa 94 wa Tuzo za Oscar, ambao wanastahili wakati huu wa kutambuliwa na wenzao na wapenzi wa filamu duniani kote.”
Sanaa inaiga maisha
Jada Pinkett Smith, ambaye pia ni mwigizaji, anaugua ugonjwa wa alopecia, na alifichua hadharani uchunguzi wa daktari kuhusu hali yake mwaka wa 2018.
Kulingana na Scott Feinberg wa The Hollywood Reporter, ambaye alihudhuria tamasha hilo, Smith aliyekuwa akitokwa na machozi alihitaji “kuvutwa kando na kufarijiwa” na waigizaji wenzake Denzel Washington na Tyler Perry wakati wa mapumziko ya hafla hiyo.
Kisha, rapa na mtayarishaji Sean ‘Diddy’ Combs, akiwasilisha sehemu inayofuata, alisema: “Will na Chris, tutasuluhisha hilo kama familia. Hivi sasa, tunaendelea kwa upendo.”
Smith, 53, alishinda tuzo ya Oscar kwa uigizaji wake kama baba wa nguli wa tenisi Venus na Serena Williams katika filamu “King Richard.”
Huku machozi yakitiririka mashavuni mwake, Smith alisema kwamba “Richard Williams alikuwa mlinzi mkali wa familia yake,” na kwamba “sanaa huiga maisha.”
“Nimeonekana kama baba mwenye kichaa, kama walivyosema kuhusu Richard Williams. Lakini mapenzi yatakufanya ufanye mambo ya kichaa,” aliongeza.
“Natumai Academy itanikaribisha tena,”Smith alisema baada ya kuomba msamaha kwa waandaji wa hafla na wateule wenzake.