Senegal: Mahakama yamhukumu mbunge wa upinzani kwa kuendelea na maandamano yaliyopigwa marufuku

Dethie Fall, mbunge wa upinzani Senegal

Mahakama ya Senegal Jumanne ilimkabidhi mbunge wa upinzani kifungo cha miezi sita jela kwa kukaidi marufuku iliyowekwa kwa maandamano wakati wa maandalizi ya uchaguzi wa wabunge na kumwachilia mbunge mwingine na washtakiwa wengine 82 waliohukumiwa katika kesi hiyo hiyo.

Wabunge Dethie Fall na Mame Diarra Fame walishtakiwa pamoja na washtakiwa wengine 82 katika mahakama ya mji mkuu Dakar.

Walikamatwa Juni 17 wakati wa maandamano yaliyoitishwa na upinzani baada ya orodha yake ya wagombea katika uchaguzi huo kuondolewa kwa sababu zisizoeleweka.

Mkutano huo ulikuwa umepigwa marufuku na mamlaka, kwa sababu ya hatari ya kuwepo machafuko.

Mapigano yalizuka huko Dakar na eneo la kusini la Casamance baada ya vijana kukaidi marufuku hiyo.

Watu watatu walifariki na wengine 200 kukamatwa, kulingana na upinzani.

Fall “mara kwa mara alikiri kuwa ndiye mratibu mkuu” wa maandamano hayo, rais wa mahakama Ahmed Ba alisema, akimpatia kifungo cha miezi sita kilichosimamishwa na faini ya franc 100,000 ($160).

Hakimu alitupilia mbali kesi dhidi ya Fame, akisema ukweli dhidi yake haujathibitishwa vya kutosha.

Ba pia aliwaachilia washtakiwa wenzake wengine 82 kutokana na “ukweli ambao haujathibitishwa vya kutosha” mwishoni mwa kesi hiyo, ambayo ilidumu kwa zaidi ya saa 14, na kumalizika mapema Jumanne.

Wafuasi, akiwemo kiongozi mkuu wa upinzani Ousmane Sonko, walikuwa wameshangilia washtakiwa walipowasili mahakamani Jumatatu asubuhi.

“Ninakataa ukweli huu wote ambao ninatuhumiwa,” Fall alisema.

“Tuko Senegal — haki ya kuandamana imewekwa kwenye katiba.”

Mbunge mwenzake Fame alisema alikamatwa baada ya yeye na watoto wake wawili kwenda kumuona kiongozi wa upinzani na meya wa Dakar Barthelemy Dias.

“Niambie kama nchini Senegal sheria zinakataza kwenda kuonana na marafiki, jamaa au watu unaowafahamu,” alisema.

Wabunge hao wawili walishutumu utekelezaji wa sheria kwa “kuwateka nyara.”

Mvutano umekuwa ukiongezeka tangu mahakama ya juu zaidi ya Senegal mnamo Juni 3 kutopitisha orodha ya wagombea wa upinzani.

Zuio hilo ilimzuia Sonko, anawania urais, kushiriki uchaguzi wa Julai 31.

Upinzani, ambao umeitisha maandamano mapya siku ya Jumatano, umetishia kuzuia kura hiyo isifanyike ikiwa orodha hiyo haitarejeshwa.

Mashirika ya kiraia yametoa wito wa kuwepo kwa mazungumzo.