Chama kikuu cha upinzani nchini Senegal kilisema kuwa kitasitisha maandamano yaliyopangwa na kushiriki katika uchaguzi ujao ambao ulikuwa umetishia kutoshiriki baada ya kuzuka kwa mzozo kuhusu wagombea wake.
Mvutano umekuwa ukiongezeka katika nchi hiyo kabla ya upigaji kura wa wabunge wa Julai 31, unaoonekana kuwa uchaguzi muhimu kwa Rais Macky Sall.
Watu watatu walikufa katika maandamano yaliyoharamishwa mnamo Juni 17, kulingana na takwimu za upinzani, na viongozi walipiga marufuku maandamano mengine yaliyoitishwa na upinzani Jumatano.
Lakini saa chache baadaye, kiongozi mkuu wa upinzani nchini humo, Ousmane Sonko, alisema maandamano hayo yanasitishwa “kufuatia ombi kutoka kwa umma, ambayo ilionyesha wasiwasi wake juu ya vurugu wakati wa tamasha la Waislamu la Tabaski” mnamo Julai 10. Watu pia walikuwa na wasiwasi kuhusu hatari hiyo ya usumbufu kwa wanafunzi wanaofanya mitihani muhimu, alisema.
“Tunapaswa kufanya mabadiliko muhimu kuelekea kujiandaa kwa uchaguzi wa wabunge wa Julai 31,” Sonko aliwaambia waandishi wa habari katika mji mkuu wa Dakar.
Muungano wa upinzani Yewwi Askan Wi “utashiriki chaguzi hizi,” na kusimamisha wagombea katika wilaya zote 54 za mkoa, alisema.
Kura hiyo ni kwa Bunge la Kitaifa lenye viti 165, ambapo wafuasi wa Sall wana wingi wa kura.
“Ikiwa Macky Sall atashindwa, hatazungumza kuhusu kuwania muhula wa tatu,”alisema Sonko, akirejelea madai ya upinzani kwamba rais huyo aliyechaguliwa mara mbili anataka kuongeza muda wake madarakani.
Sonko aliibuka wa tatu katika uchaguzi wa urais wa 2019 na tayari ametangaza kuwa atashiriki katika kura ya 2024.
Senegal ina sifa ya utulivu katika eneo ambalo machafuko ya kisiasa yameenea.
Lakini nchi ilitikiswa na ghasia za siku kadhaa mwezi Machi mwaka jana, na kusababisha vifo vya makumi ya watu baada ya Sonko kushtakiwa kwa ubakaji.
Hali ya kisiasa ilianza kuwa mbaya baada ya mahakama kuu ya Senegal mnamo Juni 3, kutoa sababu za kiufundi, kuwatupilia mbali wagombea waliowasilishwa na chama cha upinzani Yewwi Askan Wi, jina linalomaanisha “Watu Huru” kwa Kiwolof.
Wakitangaza hatua hiyo kuwa ya kisiasa, viongozi wa kundi hilo waliitisha maandamano Juni 17. Mbali na vifo hivyo vitatu, karibu watu 200 walikamatwa, upinzani ulisema.
Wabunge wawili walikuwa miongoni mwa waliozuiliwa, mmoja wao alipewa kifungo cha miezi sita siku ya Jumatatu, huku mwingine akiachiliwa.
Maandamano mengine, yaliyopangwa kufanyika Jumatano, yalipigwa marufuku na gavana wa Dakar, ambaye alitangaza kuwa kulikuwa na ‘hatari halisi’ kwamba mkutano huo ungeingiliwa na wavurugaji na utulivu wa umma na mali inaweza kuhatarishwa.