Seneta wa Marekani Chris Andrew Coons ambaye yuko nchini Kenya amekutanana na kufanya mazungumzo na rais Uhuru Kenyatta katika ikulu ya Nairobi.
Seneta huyo amempongeza rais Kenyatta kwa kuhakikisha amani inazingatiwa wakati wa uchaguzi mkuu nchini Kenya.
“Tumefurahia jinsi taifa la Kenya limezingatia amani kabla wakati na baada ya uchaguzi mkuu,” alisema seneta Coons.
Kwa upande wake, rais Kenyatta amesema Kenya itasalia imara katika kuhakikisha kuna uongozi bora nchini Kenya ndiposa iweze kuendelea kushikilia nafasi yake nzuri kama taifa ambalo linatoa mfano mwema wa kidemokrasia kwa kuzingatia amani wakati wa kubadili uongozi.
Rais Mteule William Ruto akutana na seneta Coons
Seneta huyo wa Marekani Chris Coons pia alifanya mazungumzo na rais mteule William Ruto na baadaye kukutana mpinzani wake Raila Odinga ambaye amepinga matokeo ya uchaguzi huo.
Kulingana na rais mteule, mkutano kati ya Ruto na seneta huyo uliofanyika katika makao yake ya Karen ulilenga kujadili kuimarisha ushirikiano kati ya Marekani chini ya uongozi wa Joe Biden na Nairobi.
Hata hivyo suala kuhusu uasalama baada ya uchaguzi mkuu ulifanyika agosti 9 haukukosa nafasi katika mkutano huo.
“Tumefanya mkutano na ujumbe kutoka Marekani ukiongozwa na Seneta Chris Andrew. Tulizungumzia uchaguzi ulikamilika nchini na masuala kuhusu uhusiano wa kati ya Kenya na Marekani. Tumejitolea kuimarisha uhusiano katika ya mataifa hayo mawili ndiposa raia wa Kenya na Marekani wanufaike kutokana na uhusiano wetu,” Alisema rais mteule Ruto.
Viongozi wengine wa Kenya Kwanza waliohudhuria ni pamoja na naibu rais mteule Rigathi Gachagua, Kiongozi wa chama cha Amani Musalia Mudavadi, mwenzake wa chama cha Ford Kenya Moses Wetangula, seneta wa kaunti ya Tharaka Nithi Kithure Kindiki, aliyekuwa gavana wa kaunti ya Machakos Afred Mutua na Waziri wa zamani Ababu Namwamba.
Odinga akutana na Seneta wa Marekani
Seneta Coons baada ya hapo amekutana na kiongozi wa muungano wa Azimio la Umoja Raila Odinga na kujadili na kujali masuala yanayofungamana na demokrasia.
Kulingana na mitandao ya kijamii ya Odinga viongozi hao walizungumza kuhusu uchaguzi mkuu na uhusiana kati ya Kenya na Marekani.
Odinga akisema walisistiza kutumia njia za kisheria kutatua utata ulioikumba uchaguzi mkuu.