Serikali ya Cameroon imesema watu 16 wameuawa kwenye moto katika klabu ya usiku

Serikali ya Cameroon ilisema Jumapili kuwa watu 16 waliuawa katika moto uliosababishwa na fataki katika klabu moja mjini Yaounde, mkasa huo ukitokea wakati taifa hilo likiwa mwenyeji wa mashindano ya soka ya Kombe la Mataifa ya Afrika.

“Ripoti ya awali inaonyesha watu 16 waliuawa na wengine wanane kujeruhiwa vibaya” baada ya moto kuzuka Jumamosi usiku, wizara ya mawasiliano ilisema katika taarifa.

Moto huo uliteketeza chumba kikuu cha Liv’s Night Club katika wilaya ya Bastos mjini Yaounde ambako ni mtaa wanakokaa mabalozi na wanadiplomasia wengi.

“Janga hilo lililosababishwa na milipuko ya fataki zinazotumika mara kwa mara katika maeneo haya, kwanza liliteketeza dari ya jengo hilo na kusababisha milipuko miwili mikubwa sana na kusababisha hofu na mkanyagano,” wizara hiyo ilisema.

Mlinzi aliyekuwepo moto ukianza alisema “ulitokea haraka sana.”

“Ilikuwa muda wa saa 8:00 asubuhi na wateja wengi hufika mwendo wa saa 9:00 asubuhi… kuna waathiriwa wengi,” mlinzi huyo alisema.

Cameroon ni mwenyeji wa michuano ya AFCON licha ya vurugu za mara kwa mara katika eneo la magharibi mwa nchi hiyo, ambapo wapiganaji wanaozungumza Kiingereza walitangaza uhuru kutoka kwa nchi hiyo inayozungumza Kifaransa wengi mwaka 2017.

Wanajeshi wanaotaka kujitenga na vikosi vya serikali wameshutumiwa kwa ukatili katika mapigano hayo, ambayo yamesababisha vifo vya takriban watu 3,000 na kuwalazimu zaidi ya 700,000 kukimbia makazi yao.

Takriban watu 100 walikusanyika nje ya chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya kijeshi katika kitongoji cha Ekounou cha Yaounde, wakitarajia kupata habari kuhusu jamaa zao.

 Mji mkuu wa Douala ndio kituo kikubwa cha kiuchumi ,angalau discos tano zimeteketezwa kwa kiasi au kabisa na moto katika kipindi cha miaka sita iliyopita.