Shahidi aeleza hotubu ya Lissu ilivyomshawishi kuunga mkono agenda ya “No Reform No Election”

Shahidi wa tano katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, ameendelea kutoa ushahidi wake mahakamani akieleza namna alivyojiunga na harakati za kisiasa na kushiriki katika shughuli mbalimbali za chama hicho.

Shahidi aeleza hotubu ya Lissu ilivyomshawishi kuunga mkono agenda ya “No Reform No Election”

Shahidi huyo wa siri, aliyetambulika kwa jina la P6, amesema ana umri wa miaka 24, ni Mkristo na ni mkazi wa mkoani Ruvuma, Songea, akijishughulisha na kazi ya usafirishaji kwa kutumia bodaboda.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Cuthbert Mbilinyi, shahidi huyo alidai kuwa alianza kufuatilia siasa za Chadema mwaka 2024 baada ya kuvutiwa na viongozi wa chama hicho, akiwemo Tundu Lissu.

Alieleza kuwa kupitia ufuatiliaji huo alimfahamu aliyekuwa Katibu wa Vijana Songea, anayejulikana kama Esau Chiza au maarufu kwa jina la “Mwamba wa Kigoma”. Shahidi huyo ambaye ametolea ushahidi wake kwenye kizimba cha siri, alidai kuwa Januari 2025 alichukua hatua ya kumfuata kiongozi huyo na kueleza nia yake ya kujiunga na chama.

Kwa mujibu wa maelezo yake, alipokelewa vizuri na kuahidiwa kushirikishwa katika shughuli za chama huku akisubiri kupatiwa kadi ya uanachama ambapo hakuweza kuipata kwa haraka kutokana na mashine ya kutolea kadi kudaiwa kuwa mbovu.

P6 alidai kuwa alishiriki au kuandaliwa kushiriki katika shughuli mbalimbali za chama, ikiwemo kuongoza misafara ya bodaboda yenye bendera za chama wakati wa mikutano ya hadhara ya viongozi mbalimbali wa kichama.

Akieleza tukio la Aprili 4, 2025, shahidi huyo alisema akiwa kazini na simu yake aina ya Infinix Smart 8, aliingia kwenye mtandao wa YouTube kupitia akaunti ya Jambo TV ambapo huko alikutana na hotuba ya Tundu Lissu. Alidai kuwa katika hotuba hiyo, Lissu alisikika akisema “bila mabadiliko hakuna uchaguzi” na kwamba watakwenda “kukinukisha” na “kuvuruga uchaguzi” iwapo hakutakuwa na mabadiliko.

Kwa mujibu wa shahidi, maneno hayo yalimshawishi kutamani kushiriki katika kile alichokiita agenda ya kuzuia uchaguzi wa mwaka 2025. Alifafanua kuwa alielewa “kukinukisha” kuwa na maana ya kufanya vurugu au kuzuia uchaguzi Mkuu wa 2025 unaohusisha uchaguzi wa udiwani, ubunge na urais.

Baada ya hotuba hiyo, alisema alimfuata tena kiongozi huyo wa vijana Songea na kueleza nia yake ya kushiriki katika harakati hizo, ambapo aliwekwa kwenye kundi la mtandao wa kijamii lililoitwa “Siasa Yetu Update”.

Shahidi huyo pia alieleza kuhusu maandalizi ya kumpokea Lissu mkoani Ruvuma Aprili 10, 2025, katika uwanja wa Shule ya Msingi Matawawe, Songea.

Hata hivyo, alidai kuwa Aprili 9, 2025 alipata taarifa kuwa Lissu amekamatwa wilayani Mbinga. Licha ya taarifa hiyo, alisema waliambiwa waendelee kukusanyika uwanjani, ambapo viongozi mbalimbali wa chama walitarajiwa kuhudhuria akiwemo John Heche.

Kwa mujibu wa ushahidi wake, polisi waliwasili na kuwatawanya, kisha baadaye kupiga mabomu ya machozi walipokusanyika katika ofisi za chama wakitaka kujua hatma ya mkutano huo.

Aidha, shahidi alidai kuwa Aprili 20, 2025, siku ya Pasaka, kulipangwa matembezi ya hiari Songea ambapo washiriki walitakiwa kuvaa fulana zenye ujumbe wa “No Reform No Election”.

Alisema alifika eneo lililotajwa kama “DISI Kitimoto” akiwa amevaa fulana hiyo, lakini polisi walifika na kuwakamata kwa tuhuma za kupanga maandamano bila kibali na kuwapeleka Kituo cha Polisi Songea.

Alidai kuwa baadaye walipewa dhamana na kutakiwa kuripoti ofisi ya RCO Ruvuma Aprili 25, 2025, ambapo walihojiwa kuhusu tukio hilo.

Katika hatua ya kujitetea, Tundu Lissu alimpinga shahidi huyo kwa kumwonyesha maelezo yake ya polisi yaliyopokelewa kama kielelezo cha nne mahakamani.

Lissu alionesha dosari katika maelezo hayo, ikiwemo tofauti ya dini ambapo katika maelezo ya polisi ilidaiwa ameandikwa kuwa Muislam wakati mahakamani alieleza kuwa ni Mkristo.

Lissu pia alimuuliza maswali kuhusu iwapo kauli za kisiasa kama “bila mabadiliko hakuna uchaguzi” au kuvaa fulana zenye ujumbe wa “No Reform No Election” ni makosa ya jinai, ambapo mara kadhaa shahidi alijibu kuwa hafahamu.

Aidha, alipoulizwa namna alivyobadilika kutoka kuwa mtuhumiwa wa kupanga maandamano yasiyo na kibali hadi kuwa shahidi katika kesi ya uhaini, P6 alijibu kuwa hafahamu.

Kwa sasa kesi inaendelea kwa usikilizwaji wa shahidi wa 6, ambaye si shahidi wa siri.