Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Dar es Salaam imeendelea kusikiliza ushahidi katika kesi ya Uhaini inayomkabili mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, ambapo shahidi 8 ambaye ni siri anayejulikana kwa jina la P8 alitoa maelezo yake kwa kina kuhusu chanzo cha madai ya kuhamasisha uasi.

Shahidi huyo, mwenye umri wa miaka 26, Mkristo na mkazi wa Njoro mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, alieleza kuwa ni mfanyabiashara wa matunda katika soko la Mbuyuni na kwamba anajihusisha na siasa kama mwanachama wa CHADEMA, lakini si kwa undani mkubwa.
Akijibu maswali ya Wakili Mkuu wa Serikali, Nasoro Katuga, shahidi alisema kuwa tarehe 4 Aprili 2025 alikuwa katika shughuli zake za kibiashara lakini akiwa hapo alitumia simu yake ya mkononi kuperuzi mitandaoni ambapo kupitia mtandao wa YouTube alifanikiwa kuona hotuba ya Tundu Lissu kupitia mtandao huo na mtandao mwingine wa Facebook.
Kwa mujibu wa shahidi, aliingia katika chaneli ya Jambo TV kwenye YouTube na kusikia kile alichokitaja kuwa ni tamko la mshtakiwa lililohamasisha vijana kufanya uasi iwapo hakutakuwa na mabadiliko katika mchakato wa uchaguzi wa mwaka 2025.
Wakili:Ahaa haya twende hiyo , tarehe 4 Aprili 2025 unakumbuka nini
Shahidi: Aah tarehe 4 Aprili, 2025 Nakumbuka nilikua kwenye shughuli zangu za kibiashara soko la Manyema nakumbuka nilikua niko kwenye mitandao ya Kijamii nilikua nafatilia mambo yangu, ila nilipoona hotuba ya Tundu Lissu ambaye kwa sasa mshtakiwa, nilikua YouTube na Facebook
Wakili: Uliingia huko YouTube na Facebook uliingia kupitia nini?
Shahidi: Niliingia kupitia account yangu kwa kutumia Simu Janja( Smart Phone aina ya Oppo F1x)
Wakili: Kitu gani kilikuwezesha kuingia YouTube
Shahidi: Bando langu
Wakili: Tuendelee na YouTube, uliingia kwenye Channel gani?
Shahidi: Ilikua kwenye Jambo TV
Wakili:Waambie Waheshimiwa majaji kwenye Jambo TV uliona nini?
Shahidi: Kama nilivyoeleza hapo awali niliona tamko na kusikia tamko la mshtakiwa Tundu Lissu akisema na kutuhamasisha vijana wake ya kwamba lazima tufanye uasi dhidi ya Serikali na kukinukisha tutakwenda kuvuruga uchaguzi iwapo Serikali haitafanya mabadiliko katika uchaguzi uliofanyika 2025.
Wakili: Tuambie sasa umeiambia Mahakama wewe ni mwanachama wa Chadema, ulifanya nini baada ya kuyasikia hayo?
Shahidi: Nilipata hamasa ya kuwahamasisha vijana wenzangu kulingana na kauli yake aliyosema kwamba ‘No Reform No Election
Wakili:Ebu Tuambie vitu vilivyokua vimekupa hamasa kutokana na hizo kauli za kukinukisha kuhamasisha uasi
Shahidi: Kitu ambacho kimenipa hamasa ni kutokana na ule uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka jana nakumbuka viongozi wa mitaa walikatwa na kupewa CCM kitu ambacho kiliniuma Sana
Shahidi alidai kauli hiyo ilimpa hamasa ya kuwahamasisha vijana wenzake wa mtaani zoezi ambalo alilifanya Aprili 8, 2025 katika eneo la Njoro maarufu Pepsi.Hata hivyo wakati akiendelea na zoezi hilo kuwahamasisha ghafla alikamatwa na Polisi huku wenzake wakikimbia
Wakili: Ulisema umewahamasisha watu gani?
Shahidi: Nilikua nahamasisha vijana wenzangu wa mtaani
Wakili: Unawahamasisha nini?
Shahidi: Nilikua nawahamasisha nawaambia twende tukakinukishe, tukafanye uasi.
Wakili: Ebu nikukumbushe tarehe 8 na 9 Aprili 2025 unakumbuka nini?
Shahidi: Nakumbuka nilikua kwenye zoezi langu la kuhamasihsa vijana eneo la Njoro ya Pepsi
Wakili: Ulikuwa unawahamaisha kuhusiana na nini
Shahidi: Nilikua nawahamasisha No Reform No Election
Wakili: Nini kilitokea
Shahidi: Nakumbuka tu ghafla nilikamatwa na Askari vijana wenzangu wakakimbia
Wakili: Baada ya kukamatwa na Askari nini kiliendelea?
Shahidi: Baada ya kukamatwa nilipelekwa ofisi ya RCO Moshi Kilimanjaro.
Wakili: Hapo ofisi ya RCO unakumbuka nini?
Shahidi: Nakumbuka baada ya kufikishwa pale nilikabidhiwa kwa Afande mmoja anaitwa Rashidi
Wakili: Unaweza kujua ulikamatwa kwa sababu zipi?
Shahidi: Sababu naeza kuzijua kwa sababu nilipofikishwa pale kwa RCO ilibidi nieleze ukweli wote maana niliogopa sana.
Wakili: Ulivyoenda kwa afande RCO baada ya kuulizwa ulijua makosa yako
Shahidi: Cha kwanza aliniuliza ninapoishi na kwa nini nawahamasisha vijana kufanya uasi dhidi ya Serikali.
Wakili: Alikua afande gani
Shahidi: Afande Rashidi
Wakili: Baada ya kueleza hayo nini kilifata
Shahidi: Baada ya kueleza hayo nyuma ya ofisi za RCO kuna kituo cha Polisi niliingizwa Mahabusu nilikaa masaa kadhaa.
Wakili: Baada ya kuwa umeingizwa mahabusu.
Shahidi: Nilikaa masaa kadhaa ilipofika majira ya saa 11 jioni niliachiwa kwa dhamana
Wakili: Hiyo dhamana nani alikudhamini
Shahidi: Hiyo dhamana nilijidhamini mimi mwenyewe ila kuna masharti nilipewa, nakumbuka ilikua kila mwanzo wa wiki ya Jumatatu natakiwa niripoti
Kwa mujibu wa maelezo yake, aliwekwa mahabusu kwa saa kadhaa kabla ya kuachiwa kwa dhamana ya kujidhamini, kwa masharti ya kuripoti kila Jumatatu.
Baada ya upande wa mashtaka kumaliza kumuhoji, Tundu Lissu alianza kumuuliza maswali shahidi huyo.
Katika maswali yake, Lissu alielekeza hoja kwenye maelezo ya awali aliyotoa shahidi polisi.
Shahidi alikiri kuwa baadhi ya mambo aliyoyasema mahakamani hayakuwepo katika maelezo yake ya polisi, lakini akasisitiza kuwa aliona ni muhimu kuyataja mbele ya Mahakama.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa hakudanganya polisi bali aliogopa wakati wa mahojiano ya awali.
– Mvutano na vicheko mahakamani-
Kulizuka hali ya vicheko katika ukumbi wa Mahakama pale Lissu alipomwambia shahidi kuwa yeye ni mwanachama wake, jambo ambalo shahidi alikana akikwambia kuwa yeye sio mfuasi wake akidai kuwa mambo hayo ndio yaliyomfanya kuingia katika hatia kiasi cha kufika hatua ya kutoa ushahidi Mahakamani kitu ambacho hakukitarajia.
Lissu: Kwa nini nikuchoshe wakati wewe ni mwanachama wangu?
Shahidi: Mimi sio mwanachama wako.
Katika hatua nyingine, shahidi alimjibu Lissu;
Shahidi: Mbona una maswali ya kitoto wewe mzee,” kauli iliyozua vicheko zaidi mahakamani.
Aidha, shahidi alikiri kuwa aliwahi kutishiwa kufuatia tukio hilo, lakini akaongeza kuwa anaishukuru Serikali kwa kumuacha huru.
Shahidi: Kwanza bwana naishukuru Serikali, Serikali bwana achana nayo ukweli bwana umuweka mtu huru kwa hiyo sikutaka kubishana nao kwa sababu mimi ni mdogo nina malengo yangu nashukuru nipo huru maana hata ningekataa ina mkono mrefu wangenikamata.
Awali kabla ya shahidi huyo kutoa ushahidi wake mapema leo, Mahakama ilisikiliza pia ushahidi wa shahidi wa 7 wa upande wa Jamhuri ambapo shahidi huyo wa siri alijukana kama P2, ambaye nae kimsingi alieleza namna hotuba ya Lissu ya Aprili 3,2025 ilivyomchchea yeye kushiriki katika uasi kwa kuzingatia kauli mbiu ya “No Reforms No Election”
Kesi hiyo imeahirishwa mpaka kesho ambapo shahidi wa tisa anatarajiwa kutoa ushahidi wake.
Aidha Mahakama imewaelekeza mawakili wa Serikali kuleta mashahidi watatu kuanzia kesho.