Shahidi: Kuzuia Uchaguzi ni Kosa Ndio Maana Tulikamatwa

Shahidi wa 11 katika kesi ya Uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema Tundu Lissu, amesema kuzuia uchaguzi ni kosa na ndio maana alikamatwa yeye na mwenzake.

Shahidi: Kuzuia Uchaguzi ni Kosa Ndio Maana Tulikamatwa

Shahidi huyo wa kificho wa upande wa Jamhuri anaejulikana kama P7 ameeleza hayo leo mbele ya Mahakama wakati akiulizwa maswali ya dodoso na mshtakiwa Tundu Lissu.

Pamoja na hayo Shahidi huyo mkazi wa Arusha mwenye umri wa miaka 26 amekiri kutokuwepo kwa baadhi ya maelezo ya ushahidi wake ambapo katika ushahidi aliousema Mahakamani leo, baadhi ya maelezo hakuandika katika maelezo yake ya Polisi.

Lissu:Katika ushahidi wako leo umeieleza Mahakama kwamba pale kijiweni kuna watu wengi, Mamantilie na maduka ya bidhaa za nyumbani?

Shahidi:Kweli

Lissu:Hayo maneno yapokwenye maelezo yako?

Shahidi:Hayapo.

Lissu:Vilevile umesema kwenyeushahidi wako leo, ukasema huyo mtu aliyekuja kuleta mada kijiweni kuhusu hotuba yangu alisema kwamba Chadema tutakinukisha mbaya, hayo maneno yapo kwenye maelezo yako?

Shahidi:Hakuna

Lissu:Pia ulileza kwamba huyo mtu alieleza kwamba majaji hawatendi haki kwa sababu ni vibaraka wa CCM?

Shahidi:Hayapo.

Lissu:Umesahau ulichokiandika polisi?

Shahidi:Nilikua naandika maelezo sio Kitabu.

Lissu:Kwenye ushahidi wako leo ulisema kwamba baada ya kusikia yale maneno pale kijiweni, ikabidi uingie kwenye mtandao wa YouTube kwa njia ya simu janja ili kujiridhisha kilichosemwa, Je hayo maelezo yapo kwenye maelezo yako?

Shahidi:Sijataja

Lissu:Sasa Shahidi kwenye ushahidi wako uliingia mtandaoni kwenye channel ya Jambo Tv?

Shahidi:Kweli.

Lissu:Hayo maneno uliingia kwenye mtandao wa YouTube wa Jambo Tv yapo kwenye maelezo yako?

Shahidi:Hayapo.

Mara baada ya hapo ndipo Lissu alipomuhoji Shahidi kuhusu suala la kuwa kuzungumzia uchaguzi ni kosa kisheria  lakini Lissu alikwenda mbali zaidi akitaka kujua iwapo shahidi anatishiwa au laa kiasi ambacho kimesababisha kuwa Shahidi wa kificho na haya ndio majibu yake.

Lissu:Waeleze Waheshimiwa majaji kama ni makosa kwa mujibu wa sheria za nchi hii kumuunga mkono Tundu Lissu na chama chake.

Shahidi:Mimi sijui kwa sababu sio mwanasheria.

Lissu:Mlikua mnazungumzia kuhusu masuala ya kuzia uchaguzi mlipokuwa kijiweni, sasa shahidi kwani kuzuia uchaguzi ni kosa?

Shahidi:Ni kosa ndio maana tulikamatwa .

Lissu:Waeleze Waheshimiwa majaji umekujaje mahakamani leo.

Shahidi:Kwa miguu.

Lissu:Ulitoka Arusha mpaka Dar es Salaam kwa miguu?

Shahidi:Nilipanda basi.

Lissu:Nani alikupa nauli?

Shahidi:Mwanamke wangu.

Lissu:Sasa Shahidi Waeleze Waheshimiwa majaji kama kuna kiongozi yoyote wa Chadema au mfuasi ambaye amewahi kukutishia au kukudhuru.

Shahidi:Sijawahi kutishiwa kwa  sababu hamna mtu anaenijua.

Lissu:Unajua kwanini umepewa jina la P7?

Shahidi:Ndio.

Lissu:Kwanini?

Shahidi:Kwa ajili ya usalma wangu.

Lissu:Si umesema hujatishiwa?

Shahidi: Ndio

Awali akiongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali Thawabu Issa Shahidi P7 ambaye ni dereva bajaji aliieleza Mahakama jinsi alivyokamatwa hadi yeye kuwa miongoni mwa mashahidi 30 wa Jamhuri ambapo pamoja na mambo mengine alieleza alivyoshawishika na kauli ya Tundu Lissu kuhusu kutaka kukinukisha na kuvuruga uchaguzi.

Alieleza kuwa Aprili 3, 2025 akiwa kwenye kijiwe cha bajaji ambacho anapaki bajaji yake, alikuja mtu ambaye ni dereva mwenzao kijiweni hapo ambaye kimsingi ni shahidi aliyekwishatoa ushahidi kwenye kesi hii anaejulikana kama P4, alikuja na mada kuhusiana na alichokisema Tundu Lissu kupitia mkutano wake na wanahabari.

Mtu huyo ambaye ndiye P4 kwa mujibu wa shahidi huyo alipofika kijiweni hapo alisema “Mmesikia alichokisema Tundu Lissu, amesema watakinukisha na kuuvuruga uchaguzi”

Wakili:Unajishughulisha na nini katika maisha yako ya kila siku?

Shahidi:Naendesha Bajaji.

Wakili:Hiyo shughuli unaifanyia wapi?

Shahidi:Naifanyia kwa Mromboo Arusha.

Wakili:Shughuli hizo umezifanyia kwa muda gani sasa?

Shahidi:Toka 2023.

Wakili:Sasa Shahidi ebu iambie Mahakama, hali ya hilo eneo unalofanyia kazi ni ya namna gani?

Shahidi:Hilo eneo limechangamka kwa sababu kuna Mamantile, Maduka ya mahitaji ya nyumbani na kijiwe cha bajaji .

Wakili:Sasa Shahidi iambie Mahakama tarehe 3 Aprili, 2025 jioni ulikua wapi?

Shahidi:Nakumbuka tarehe 3 Aprili 2025, majira ya jioni nilikua maeneo ya kazini kwangu kijiweni ninakopaki bajaji kwa Mromboo Arusha.

Wakili:Ukiwa eneo hilo nini kiliendelea?

Shahidi:Tulikua kwenye mazungumzo ya kawaida ya kijiweni, baada ya hapo kuna mtu mmoja akaibua mazungumzo mengine tofauti na yale ya Mwanzo., akasema hivi hamjasikia kwamba Chadema watazuia uchaguzi wa mwaka huu.

Wakili:Kwa hiyo mtu aliyekuwa amezua mazungumzo mapya nini kiliendelea?

Shahidi:Huyo mtu akasema tena watakinukisha mbaya.

Wakili:Baada ya hapo nini kiliendelea?

Shahidi:Akasema kwamba Polisi wanaiba kura, akasema kwamba hata ukienda Mahakamani hutapata haki.

Wakili:Nini kiliendelea baada ya hayo mazungumzo?

Shahidi:Akaendelea kusema kwamba haya ukienda Mahakmani hutapta haki kwa sababu majaji ni vibaraka wa CCM, akaendelea kusema mwaka 2024 tume ya uchaguzi ilipewa maelekezo ya kukata wajumbe wa Chadema. Tukiwa tunaendelea nilipata hamasa kupitia yale maneno.

Wakili:Baada ya kusikia wewe ulifanyaje?

Shahidi:Baada ya kusikia ikabidi na mimi niingie kwenye mtandao wa YouTube nikafungua channel inaitwa Jambo Tv.

Wakili:Uliingiaje huko YouTube?

Shahidi:Nilitumia simu yangu janja.

Shahidi huyo alieleza kuwa wakati akiwa hapo na kutaka kujiridhisha kuhusiana na hayo gafla walikuja watu waliojitambulisha kuwa ni AAskari ambapo walimuweka chini ya ulinzi japo wenzake walikimbia.

Mara baada ya kukamatwa alipelekwa katika kituo cha Polisi cha Murieti na baadae kupelekwa ofisi ya RCO ambapo huko alihojiwa na kuchukuliwa maelezo akiambiwa anatuhumiwa kwa kosa la kutaka kufanya vurugu.

Shahidi P7 anafikisha idadi ya mashahidi 11 wa upande wa Jamhuri huku kukiwa na vielelezo 10 kama ushahidi Mahakamani Lissu anakabiliwa mashtaka ya Uhaini ambayo adhabu yake ni kifo kwa mujibu wa sheria za Tanzania.

Alikamatwa kwa mara ya kwanza Aprili 9,2025 huko Mbinga mkoani Ruvuma mara tu baada ya kumaliza mkutano wake wa hadhara uliokua na ajenda ya kunadi sera ya “No Reforms No Election”.

Alisafirishwa hadi Dar es Salaam na kufikishwa Mahakama ya Kisutu Aprili 10, 2025 na kusomewa mashtaka hayo.Hadi sasa ana zaidi ya siku 320 gerezani tangu akamatwe.

Kesi hiyo imeahirishwa mpaka kesho Februari 18,2025 saa tatu asubuhi ambapo upande Jamhuri unatarajiwa kuwa na mashahidi 3.