Shahidi wa 10 wa Jamhuri ameieleza Mahakama sababu zilizomfanya kutoa ushahidi wake akiwa kwenye kizimba cha siri, akidai kuwa anahofia usalama wa maisha yake.

Shahidi huyo, mkazi wa Arusha na dereva wa bajaji anayefanyia kazi eneo la Mromboo, aliongozwa kutoa ushahidi wake na Wakili wa Serikali, Winiwa Kasala.
Akijibu maswali ya awali, shahidi aliiambia Mahakama kuwa tarehe 3 Aprili 2025 majira ya saa sita mchana akiwa anasubiri abiria, aliingia kwenye mtandao wa YouTube kupitia simu yake na kukutana na taarifa kuhusu Mwenyekitiki wa Chadema Tundu Lissu.
Alidai kuwa katika video hiyo, Lissu alisikika akieleza kuwa wamejipanga kuzuia uchaguzi na kwamba “watakinukisha” kutokana na kukosa imani na mchakato wa uchaguzi. Shahidi alidai kuwa maneno hayo yalikuwa na ushawishi kwake.
“Yale maneno yaliweza kunishawishi, hasa kutokana na hali ngumu ya maisha,” alidai shahidi mahakamani.
Baada ya hapo, aliendelea na kazi yake ya kusafirisha abiria kabla ya kurejea kijiweni Mromboo, ambako alikuta mjadala ukiendelea kuhusu hotuba hiyo.
Alidai kuwa baadhi ya watu walikuwa wakiunga mkono kauli hizo wakisema huenda “kukinikisha” kungeweza kuleta nafuu ya maisha.
Shahidi alidai kuwa baada ya takribani dakika 20, askari polisi walifika eneo hilo na kuwaweka chini ya ulinzi.
Alisema baadhi ya watu walijaribu kukimbia lakini yeye na mwenzake aliyemtaja kwa kifupi kama P7 walikamatwa.
Alieleza kuwa walipelekwa Kituo cha Polisi Muriet kabla ya kuhamishiwa Kituo Kikuu cha Polisi (Central).
Huko waliambiwa wanatuhumiwa kwa kosa la kuzuia uchaguzi, wakaandikiwa maelezo na kuwekwa mahabusu.
Baadaye walipewa dhamana na kutakiwa kuripoti polisi kila siku hadi Aprili 17, 2025, kabla ya kuambiwa wasiondoke kwa kuwa kulikuwa na maelezo ya ziada.
Hata hivyo, alidai hakuwahi kufikishwa mahakamani kwa kesi hiyo wala hajui hatima ya tuhuma hizo.
Katika hatua ya maswali ya utetezi, Tundu Lissu alimuhoji shahidi kuhusu mazingira ya kufika Dar es Salaam kutoa ushahidi.
Shahidi alikiri kuwa alipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kama wakili wa Serikali akimtaka afike jijini humo, lakini hakutaja jina lake.
Alisema alijilipia nauli yake binafsi kwa kuwa alikuja Dar es Salaam kwa shughuli zake, huku akieleza kuwa siku ya ushahidi alifika mahakamani kwa gari la wanasheria.
Alipoulizwa iwapo aliwahi kutishiwa na kiongozi au mwanachama wa CHADEMA kutokana na kesi hiyo, shahidi alijibu kuwa hajawahi kutishwa wala ndugu zake.
Hata hivyo, alipoulizwa sababu ya kutoa ushahidi akiwa amejificha kwenye kizimba cha siri, alisema: “Nahofia maisha yangu pia.”
Katika maswali zaidi, alikiri kuwa hakuiwasilisha mahakamani video aliyodai kuiona YouTube, na kwamba aliitazama kupitia kile alichokiita “Habari 24”.
Kesi hiyo imeahirishwa mpaka kesho ambapo upande wa Jamhuri wanatarajia kumleta shahidi wa 11 na wengine.
Lissu mwanasiasa maarufu nchini Tanzania na Wakili mbobevu, ameshtakiwa kwa kosa la Uhaini kosa ambalo halina dhamana na hukumu yake ni kifo