Shahidi wa Jamhuri anayelindwa kwa utambulisho wa kificho kama P9 amedai mbele ya mahakama kuwa ametishiwa na watu aliowataja kuwa ni wafuasi na wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kufuatia uamuzi wake wa kufika kutoa ushahidi katika kesi inayomkabili Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu.

Akijibu maswali ya dodoso, P9 (35) anayefanya kazi ya ufundi umeme na mkazi wa jijini Mbeya, alidai kuwa kuna wanachama au wafuasi wa CHADEMA wanaofahamu kuwa anakuja kutoa ushahidi na kwamba walimtishia kwa kumwambia kuwa “lolote baya linaweza kumkuta.”
Hata hivyo, alipoulizwa majina ya waliomtishia, alikataa kuyataja akieleza ni kwa sababu za usalama wake.
Lissu: Kuna Mwanachama yoyote wa Chadema au mfuasi wa Chadema anaejua kwamba wewe unakuja kutoa ushahidi?
Shahidi: Ndio
Lissu:Walikutishiaje
Shahidi:Kama unaenda kutoa ushahidi lolote baya linaweza nikakuta
Lissu:Hao waliokutishia ni akina nani? Unaweza kuwataja kwa majina?
Shahidi:Siwezi kuwataja kwa sababu za usalama
Lissu:Ulitoa taarifa Kituo cha Polisi?
Shahidi:Ndio
Lissu:Wapi?
Shahidi:Nilitoa kituo cha Polisi Ilonga
Lissu: Waeleze Waheshimiwa majaji kama ulipewa kitu kinaitwa RB?
Shahidi:Ndio nilipewa
Lissu: Waeleze Waheshimiwa majaji kama kuna yeyote aliyekamatwa
Shahidi: Hapana
Lissu: Waeleze Waheshimiwa majaji kama kuna yeyote aliyefikishwa Mahakamani
Shahidi huyo aliiambia mahakama kuwa alitoa taarifa katika Kituo cha Polisi Ilonga na kupewa namba ya kumbukumbu ya tukio (RB), lakini alikiri kuwa hakuna mtu yeyote aliyekamatwa wala kufikishwa mahakamani kuhusiana na madai hayo ya vitisho.
Kabla ya hayo kuibuka Lissu alimtaka shahidi kuthibitisha kama aliandika maelezo Polisi tarehe 22 Aprili 2025. P9 alikubali na alipokabidhiwa nakala ya maelezo yake alithibitisha kuwa ni yake.
Hata hivyo, maswali ya utetezi yaliibua tofauti kadhaa kati ya maelezo ya awali aliyoyatoa Polisi na ushahidi wake wa mdomo mahakamani.
Wakati akitoa ushahidi wake wa awali mbele ya Wakili wa Serikali, P9 alijitambulisha kuwa ni mkazi wa Mbeya anayejishughulisha na kazi za ufundi umeme, akidai alisomea taaluma hiyo katika Chuo cha VETA Mbeya kuanzia mwaka 2008 hadi 2010. Alisema hana sehemu maalum ya kazi bali hufanya kazi popote anapoitwa ndani ya Halmashauri ya Mbeya.
Lakini alipoonyeshwa maelezo yake ya Polisi, ilibainika kuwa ameandikwa kuwa ni mkulima, jambo alilolikubali mahakamani.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Cathbert Mbilingi jana Februari 19 kabla ya kuahirishwa kwa kesi, P9 alidai kuwa tarehe 3 Aprili 2025 majira ya usiku akiwa nyumbani alikuwa akiperuzi mitandao ya kijamii kupitia simu yake aina ya Samsung 8 Pro, alisema aliingia Instagram na kuona picha na video, ikiwemo video aliyodai kumuonesha Lissu akihutubia ndani ya ukumbi.
Kwa maelezo yake, katika video hiyo kulikuwa na bendera ya CHADEMA nyuma ya Lissu, ambaye alidai alikuwa amevaa mavazi ya kombati ya kaki na fulana nyeusi. P9 alidai katika hotuba hiyo Lissu alihamasisha kufanya vurugu na kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 wa Rais, Wabunge na Madiwani.
Alisema kama mfuasi wa chama alihamasika na maudhui hayo, na kwamba tarehe 4 Aprili 2025 alijadiliana na watu anaoshi nao kuhusu kile walichokiona mtandaoni.
P9 alidai kuwa tarehe 5 Aprili 2025 alipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kama mteja wa kazi ya umeme, ambaye alikubaliana nae wakutane eneo la Mwanjelwa ili waweze kufatana kwa ajili ya kufanya kazi hiyo.
Baada ya kufika eneo walilokubaliana hali haikua kama walivyokubaliana kwani mtu huyo alijitambulisha kuwa ni askari kutoka Kituo cha Polisi Mwanjelwa na kumuonesha kitambulisho cha kazi, kisha kumueleza kuwa yupo chini ya ulinzi kwa kosa la uchochezi wa kuzuia uchaguzi.
Alisema baadaye aliachiwa kwa dhamana kwa masharti ya kuripoti kila Jumatatu. Aidha, tarehe 22 Aprili 2025 alidai alipigiwa simu na askari aliyemtaka kufika kituoni kuandika maelezo kama Shahidi katika kesi ya Lissu.
Kesi inaendelea