Shirika la Afya Duniani (WHO) Jumapili lilitangaza kuwa limetoa dozi bilioni 1 za chanjo ya UVIKO-19 kupitia mpango wake wa kimataifa wa COVAX.
Kulingana na shirika la afya linaloungwa mkono na Umoja wa Mataifa, shehena ya hivi majuzi ya chanjo milioni 1.1 ya UVIKO -19 iliyokuwa ikipelekwa Rwanda ilijumuisha dozi ya bilioni moja ya chanjo iliyotolewa kupitia COVAX.
WHO imewasilisha chanjo kwa nchi wanachama 144 kufikia sasa.
Licha ya hatua hiyo muhimu, WHO ilikiri bado wanahatua kubwa ya kupiga ili kuhakikisha kuwa watu katika nchi wanachama wanachanjwa. Kufikia sasa nchi wanachama 36 wamechanja chini ya asilimia 10 ya watu wao na wanachama 88 wamechanja chini ya asilimia 40.
“Azimio la COVAX la kusambaza chanjo hizo liliathiriwa na kujilimbikizia kwa chanjo hizo kati ya nchi tajiri, milipuko ya janga ilisababisha mipaka kufungwa. Kukosa kugawana leseni ya kuzalisha chanjo pamoja na teknolojia kutoka kwa makampuni ya dawa ilimaanisha uwezo wa kuzalisha chanjo hizo muhimu ulienda kwa kasi ndogo,WHO ilisema.
Suala la kujilimbikizia chanjo miongoni mwa mataifa tajiri limesababisha mzozo wa mara kwa mara kati ya mashirika ya afya duniani, ikiwa ni pamoja na WHO.
Mkurugenzi mkuu wa shirika la WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, mara kwa mara alitoa wito wa kusitishwa kwa watu kutoka mataifa tajiri kupata chanjo za ziada huku nchi za kipato cha chini na cha kati zikihangaika kuwachanja watu wao.
Wakati wa mkutano na waandishi wa habari mwishoni mwa Desemba, Ghebreyesus alilaumu “umaarufu na utaifa finyu” ambao ulihatarisha juhudi za kukabiliana na kuibuka kwa virusi vipya kama vile kirusi cha omicron ambacho kimeenea kwa haraka katika mataifa mengi.