Serikali ya Sierra Leone imefutilia mbali msamaha kwa mganga mmoja mashuhuri aliyehukumiwa kifo mwaka 2016 kwa kumuua na kumkatakata DJ.
Ofisi ya Rais Julius Maada Bio ilisema Jumatatu kwamba ilikuwa imebatilisha mara moja msamaha uliotolewa kwa Baimba Moi Foray, mganga wa kienyeji mnamo Januari 1.
Hatua hiyo ilifuatia shinikizo kutoka wa raia wa taifa hilo la Afrika Magharibi, ambapo mwaka wa 2015 mauaji ya kutisha ya DJ Clef, jina kamili — Sydney David Buckle – yalizua kilio nchini humo.
Katika usiku wa mwisho wa maisha yake, DJ Clef alicheza nyimbo za utata nyumbani kwa Foray, mganga maarufu nchini Sierra Leone.
Clef alipatikana baadaye viungani mwa mji mkuu wa Freetown akiwa amefariki, huku viungo vyake na sehemu zake za siri zikiwa hazipo.
Foray na mshirika wake walitiwa hatiani kwa mauaji yake mwaka uliofuata na kuhukumiwa kunyongwa kwa uhalifu wao.
Hata hivyo, kulikuwa na madai kwamba polisi walivuruga uchunguzi huku kukiwa na shauku kubwa ya vyombo vya habari na shinikizo la aliyehusika na mauaji hayo kukamatwa.
Haijulikani ni kwa nini serikali ya Sierra Leone ilimsamehe Foray mwezi huu, lakini ilisema Jumatatu kwamba itapitia upya mchakato wa kutoa msamaha.
Siku ya Jumanne, Bio pia aliteua waziri mpya wa haki, bila kutoa maelezo.
Picha zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zilimuonyesha Foray, baada ya kuachiliwa, akiwa na waziri wa zamani wa haki Anthony Brewah na Waziri wa Habari Mohamed Rahman Swaray.
Swaray alisema kwenye mtandao wa kijamii Jumanne kwamba mkutano wao na mganga huyo ulikuwa tu kwa bahati mbaya tu.
Polisi wa Sierra Leone hawakuweza kuthibitisha kwa AFP iwapo Foray alirudishwa gerezani baada ya rais kubatilisha msamaha wake siku ya Jumatatu.
Sierra Leone ilipiga marufuku adhabu ya kifo mwezi Oktoba.