Siku ya Mbivu na Mbichi Chadema ni Leo!

Leo ni siku ya mbivu na mbichi ndani ya CHADEMA! Baada ya vuta ni kuvute za muda mrefu katika kampeni, leo sanduku la kura linaamua nani awe Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Kati ya wapinzani wakuu mwenyekiti wa sasa Freeman Mbowe na Makamu wake Tundu Lissu. Mgombea wa tatu ni Charles Odero, ambaye wachambuzi wa siasa wanahoji hana nafasi kamwe ya kuwa mwenyekiti.

 

Kumekuwa na hofu huenda Chadema ikapasuka kufuatia maneno makali kutoka haswa kwa wanaomuunga mkono Lissu. Wanadai iwapo Lissu atabwagwa, basi watajiondoa chamani.

Freeman Mbowe ameomba achaguliwe tena kukiongoza chama hicho. Wajumbe wa Mkutano Mkuu 1,328 ndiyo wamebeba si tu nafasi za watatu kisiasa, bali pia kinachotajwa hatima ya CHADEMA.

 

Kati ya wajumbe hao, ni 792 ni kutoka majimbo la uchaguzi, 124 wilaya za kichama, 68 mikoa ya kichama, 30 kanda za kichama, 99 wa mabaraza na 15 wa Kamati Kuu. Wote watawachagua Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti Bara na Zanzibar.

Baadhi ya sababu zinazotolewa na wanaomuunga mkono Mbowe wanasema ni mbunifu, ndiyo sababu chama hicho kinaendelea kuwa imara kwa miaka mingi.

 

Baadhi ya hoja ambazo zimekuwa zikitolewa na wafuasi wanaomuunga mkono Lissu ni pamoja na mvuto alionao kutokana na sera zake zinazolenga mabadiliko ya kweli ndani ya chama na taifa lake.

 

Lissu, pamoja na mambo mengine, ameahidi kushusha fedha za ruzuku ya chama hadi ngazi ya majimbo, ukomo wa madaraka hasa kwenye nafasi za ubunge wa viti maalumu na ujasiri wa kupambana na vitendo vya rushwa ndani na nje ya chama chake.

 

Katika nyakati za lala salama jana, akifungua mkutano wa Baraza Kuu uliofanyika Dar es Salaam, Mbowe aliendelea kusisitiza kuwa hakuna mkubwa kuliko chama hicho huku akiwatahadharisha wanachama wasitoe nafasi kwa yeyote mwenye nia ya kukipasua chama hicho.

 

“Tusitoe nafasi kwa yeyote mwenye dhamira ya kukipasua chama, tumesema na ninarudia chama hiki kina thamani kuliko yeyote miongoni mwetu, kwani kimebeba ndoto za watanzania.

 

“Kwa hiyo ndugu zangu wana-CHADEMA, tumekuja Dar es Salaam si kupaniana, tumekuja kuyajenga, kwamba chama hiki tutakipigania, tutakijenga, tutakipanga, tunapotofautiana tutazungumza, ili mwisho wa siku kikabebe ndoto ya taifa letu ya haki, demokrasia kwa kila mmoja na hatimaye maendeleo ya watu wetu wote,” alisema.