Sudan imejipata katika mgogoro baada ya jeshi kuchukua uongozi wa nchi na kutangaza hali ya hatari.
Upinduzi wa serikali ya mpito umeondoa matumaini ya mabadiliko ya amani ya uongozi hata baada ya kuondolewa madarakani kwa aliyekuwa Rais Omar al-Bashir mwaka wa 2019.
Sudan imekuwa ikiongozwa na serikali ya muungano kwa ushirikiano kati ya jeshi la serikali na makundi ya kiraia kutoka 2019 . Ila Jumatatu, jeshi lilichukua uongozi, na kuvunja makubaliano yake na Forces for Democratic Change walioongozwa kwa pamoja serikali ya mpito.
Siku ya Jumanne kwenye hotuba yake kwa vyombo vya habari, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan,mkuu wa majeshi ya Sudan alisema kuwa Waziri mkuu Abdalla Hamdock alikuwa nyumbani kwake, na alikuwa huru kuondoka mara tu ya hali ya utulivu itakaporejea.
“Tulikaa pamoja jana, yuko na mimi nyumbani, hakukamatwa na hakuna yeyote amemjeruhi na atarudi nyumbani atakapohisi yupo salama.” Burhan aliviambia vyombo vya habari kwenye hotuba yake mjini Khartoum.
kufikia Jumanne jioni 26 OKtoba, Abdalla Hamdok na mkewe waliruhusiwa kuenda nyumbani, ila watakakuwa chini ya ulinzi.
Jumatatu, Burhan alisema makubaliano kati ya jeshi na makundi ya kiraia kuhusu baraza la serikali ya mpito ilileta mgogoro katika kipindi cha miaka miwili na kuhatarisha amani na umoja wa Sudan. Burhan amesema kuwa ibara kadhaa za katiba zimesitishwa na magavana wa majimbo kuondolewa.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, Umoja wa Afrika na Umoja wa nchi za Kiarabu siku ya Jumatatu walilaani mapinduzi na kutaka kuachiwa mara moja kwa Waziri mkuu na maafisa wengine na kurejeshwa kwa uongozi wa kiraia.
Katika hotuba kwa vyombo vya habari, ikulu ya White House imesema kuwa serikali ya Rais Joe Biden “imeshtushwa na matukio” Sudan, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisema inasitisha msaada wa kifedha wa dola milioni 700 kwa nchi hiyo.Huku Uingereza ikitaja mapinduzi kuwa “usaliti kwa watu wa Sudan”
Maelfu ya waandamanaji wanaopinga mapinduzi waliendelea kuandamana katika mji mkuu Khartoum Jumatatu na Jumanne. Takriban waandamanaji 7 wameuawa na wengine 140 kujeruhiwa kutoka Jumatatu.