Vikosi vya usalama vya Sudan vilifyatua gesi ya kutoa machozi Ijumaa kwa mamia ya waandamanaji ambao waliandamana kwa siku ya pili mfululizo katika mji mkuu kupinga mapinduzi ya kijeshi ya mwaka jana.
Waandamanaji walikusanyika tena karibu na ikulu ya rais mjini Khartoum siku moja baada ya takriban watu tisa kuuawa wakati wa maandamano ya kupinga unyakuzi wa kijeshi ulioongozwa na mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan Oktoba mwaka jana.
“Watu wanataka kumuondoa Burhan,” wanaharakati waliimba huku wengine, wakiwa wamebeba picha za watu waliouawa katika ghasia zinazohusiana na maandamano, wakipiga kelele: “Tunatoa wito wa adhabu ifanyike!”
Idadi ya vifo kutokana na ghasia zinazohusiana na maandamano imefikia 113 tangu mapinduzi hayo, huku kifo cha hivi punde kiliripotiwa Ijumaa baada ya muandamanaji kufariki kutokana na majeraha katika maandamano ya Juni 24, kulingana na matabibu wanaounga mkono demokrasia.
Wakati huo huo polisi wa Sudan walishutumu waandamanaji kwa kuwajeruhi polisi 96 na maafisa wa kijeshi 129, “wengine vibaya,” siku ya Alhamisi, pamoja na kuharibu magari na kuchoma moto.
Ukandamizaji wa siku ya Alhamisi ulikaidi wito wa jumuiya ya kimataifa ukizitaka mamlaka za Sudan kujiepusha na ghasia.
“Vurugu zinapaswa kukomeshwa,” alidai mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa Volker Perthes.
Mwanadiplomasia mkuu wa Marekani Lucy Tamlyn alisema “anatiwa wasiwasi sana” na ripoti ya vifo vya waandamanaji na “matumizi ya risasi moto ya waandamanaji na nguvu kupita kiasi dhidi ya wataalamu wa matibabu.”
Mapinduzi ya mwaka jana yaliitumbukiza Sudan katika machafuko makubwa ambayo yamesababisha kupanda kwa bei ya bidhaa na uhaba wa chakula unaotishia maisha na kusababisha maandamano ya karibu kila juma pamoja na mapigano ya kikabila.
Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na kambi ya kikanda IGAD wamejaribu kuwezesha mazungumzo kati ya majenerali na raia, lakini yamesusiwa na makundi makuu ya kiraia.
Siku ya Ijumaa, vyombo hivyo vitatu kwa pamoja vililaani ghasia na “matumizi ya nguvu kupita kiasi na vikosi vya usalama na ukosefu wa uwajibikaji kwa vitendo kama hivyo, licha ya ahadi za mara kwa mara kutoka kwa mamlaka.
Maandamano hayo Alhamisi yalikuja katika ukumbusho wa mapinduzi ya mwaka 1989 ambayo yaliiangusha serikali ya mwisho iliyochaguliwa ya kiraia ya Sudan na kuanzisha miongo mitatu ya utawala wa Jenerali Omar al-Bashir anayeungwa mkono na Waislamu.
Ilikuwa pia siku ya kumbukumbu ya maandamano ya 2019 ya kutaka majenerali waliomwondoa Bashir katika mapinduzi ya ikulu mapema mwaka huo kuachia madaraka kwa raia.
Maandamano hayo yalipelekea kuundwa kwa serikali ya mpito ya kiraia na kijeshi ambayo ilipinduliwa katika mapinduzi ya mwaka jana.