Takriban watu 20 wameuawa katika mauaji mapya katika jimbo la Ituri mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, mfuatiliaji alisema Jumatatu, na kuongeza kuwa wanamgambo wa ADF wanashukiwa kuhusika na mauaji hayo.
Shambulio hilo lilitokea usiku katika kijiji cha Bwanasura katika eneo la Irumu, Shirika la Kivu Security Tracker (KST) lilisema kwenye Twitter.
David Beiza, mkuu wa Msalaba Mwekundu huko Irumu, alisema watu wa kujitolea kutoka shirika lake “wamehesabu miili 36” katika eneo la mauaji hayo.
Ituri na jimbo jirani la Kivu Kaskazini yanapambana na mashambulizi ya makundi yenye silaha, mengi yakiwa ni urithi wa vita kutoka mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
KST ilisema kundi la Allied Democratic Forces (ADF) — kundi liitwalo Islamic State inaelezea kama washirika wake — lilishukiwa kuhusika na mauaji hayo.
Beiza alisema “Waasi wa ADF walifika mwendo wa saa nane mchana. Kwa bahati nzuri, wakazi wengi waliweza kukimbia.”
Dieudonne Malangay, kiongozi wa mashirika ya kiraia katika wilaya ya Walese Vonkutu alisema jeshi ‘lilichelewa’ kujibu.
Siku ya Jumatatu, waasi wa M23 walishambulia kwa bomu kituo cha jeshi huko Bugusa katika eneo la Rutshuru Kivu Kaskazini na kuua wanajeshi wawili na kujeruhi watano, jeshi lilisema katika taarifa.
Taarifa hiyo iliyotiwa saini na msemaji wa gavana wa kijeshi Jenerali Sylvain Ekenge ilidai kuwa Rwanda ilisambaza silaha kwa waasi.
“Matumizi ya silaha yanaonyesha msaada ambao M23 inapokea kutoka kwa mshirika wake wa asili,” jenerali huyo alisema.
Mapigano yalizuka mwezi Mei kati ya jeshi na M23, kundi ambalo kimsingi ni la Watutsi wa Congo.
Kinshasa mara kwa mara imekuwa ikiishutumu Kigali kwa kuunga mkono M23, ingawa Rwanda imekanusha shtaka hilo.
Rais wa Congo Felix Tshisekedi siku ya Jumapili alisema ‘hana shaka’ juu ya uungaji mkono wa Rwanda kwa waasi, lakini anatumai kutakuwa na uhusiano mzuri na Kigali.
ADF imekuwa ikilaumiwa kwa mauaji, utekaji nyara na uporaji tangu 2013, na idadi ya vifo inakadiriwa kuwa kwa maelfu.
Ituri na Kivu Kaskazini zimekuwa chini ya ‘hali ya kuzingirwa’ tangu Mei mwaka jana — hatua inayowaweka wakuu wa jeshi katika nyadhifa za mamlaka ili kuharakisha juhudi za kuimarisha usalama.
ADF pia walilengwa katika operesheni ya pamoja iliyoanzishwa mwezi Novemba mwaka jana na vikosi vya serikali na Uganda kufuatia mashambulizi ya mabomu katika mji mkuu wa Uganda Kampala.
Operesheni hiyo ambayo ilipaswa kukamilika Mei 31, imeongezwa muda kwa miezi miwili.