Takriban watu sita walikufa, akiwemo msichana mdogo, na karibu wengine 50 waliokolewa baada ya mashua ya wahamiaji iliyojaa mizigo kupinduka kaskazini mwa Lebanon wakati wa msako uliofanywa na vikosi vya wanamaji, maafisa wa Lebanon walisema Jumapili.
Boti iliyokuwa imebeba takriban watu 60 ilipinduka usiku wa kuamkia Jumamosi karibu na mji wa bandari wa Tripoli, eneo ambalo idadi kubwa ya wahamiaji wasio halali hututmia kusafiri kuenda Ulaya.
Ajali hiyo, imefanyika kabla ya uchaguzi wa bunge uliopangwa kufanyika Mei 15,na sio ajali ya kwanza ya aina yake kwa nchi hiyo iliyokumbwa na mzozo na inayokabiliana na mdororo mbaya zaidi wa kifedha kuwahi kutokea.
“Vikosi vya wanamaji vya jeshi hilo vilifanikiwa kuwaokoa watu 48 na kuopoa maiti ya msichana… kutoka kwenye boti iliyozama wakati ikijaribu kuwatorosha wahamiaji kwenda ulaya kinyume cha sheria,” ilisema taarifa ya jeshi hilo.
“Watu wengi waliokuwa kwenye meli waliokolewa,” jeshi lilisema, bila kutaja mataifa ya wahamiaji hao.
Jeshi lilitoa maiti watano kwenye pwani ya Tripoli siku ya Jumapili, Shirika rasmi la Habari la Taifa liliripoti, saa chache baada ya mwili wa msichana mdogo kurejeshwa ufukweni.
Vilio vya jamaa vilisikika kutoka katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Tripoli ambako maiti walikuwa wamehifadhiwa.
Makumi ya watu walitazama huku kundi la wanaume walipovamia chumba cha kuhifadhia maiti na kutoa maiti ya mwathiriwa kwa ajili ya mazishi, mwandishi alisema.
Nje, makumi ya vijana walirusha mawe kwenye vifaru viwili vya jeshi na katika kizuizi cha karibu cha jeshi, na kusababisha askari kufyatua risasi hewani.
Katika bandari ya Tripoli, jamaa za waliopotea walisubiri kwa hamu habari za wapendwa wao.
“Mpwa wangu, ana watoto watano na mke wake ana mimba ya mapacha. Alikuwa akijaribu kuepuka njaa na umaskini,” mwanamume mmoja alisema.
Haissam Dannaoui, mkuu wa jeshi la wanamaji la Lebanon, alisema mashua ya mita 10 (futi 33) iliyojengwa mwaka 1974 ilikuwa na wahamiaji karibu 60 na ilisafiri baharini bila tahadhari zozote za usalama, aliambia mkutano wa waandishi wa habari.
Dannaoui alisema jeshi lilijaribu kuzuia mashua hiyo kusafiri nje ya eneo la Qalamoun, kusini mwa Tripoli, lakini haikuweza kufikia mashua hiyo kwa wakati.
Msako wa baharini ulifuata huku doria mbili za majini zikijaribu kulazimisha mashua ya wahamiaji kurejea ilikotoka.
“Boti ya doria ilitugonga mara mbili… ili kutuzamisha,” mwanamume huyo aliambia AFP bandarini.
Mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon Najat Rochdi alitoa wito wa kukomeshwa kwa majanga haya ya mara kwa mara.
“Inatisha kuona umaskini bado unasukuma watu kuchukua safari ya hatari kuvuka bahari,” alisema kwenye Twitter.