Takriban watu 91 wauawa baada ya lori la mafuta kulipuka

Takriban watu 91 wameuawa na wengine 100 wamejerihiwa mjini Freetown Jumamosi baada ya lori la mafuta kulipuka baada ya kugongana na lori jingine.

Mamlaka nchini Sierra Leone hawajatoa taarifa rasmi kuhusu idadi ya wale waliouawa katika mkasa huo ila meneja wa mochauri ya serikali Sinneh Kamara amesema wamepoeka mili 91 kufuatia mlipuko huo. Waathiriwa 100 wamepelekwa katika hospitali tofauti mjini Freetown, amesema Naibu Waziri wa afya Amara Jambai.

Picha zilizowekwa mitandaoni zimeonyesha miili ya watu walioungua barabarani na moto huo ulivyoenea hadi katika maduka na nyumba zilizokuwa karibu na eneo la mkasa.

Rais wa Sierra Leone Julius Maada Bio alisema kwenye taarifa yake kwenye Twitter “Nimesikitishwa sana na moto huo mbaya na vifo vya kutisha vya watu. Serikali yangu itafanya kila iwezavyo kusaidia familia zilizoathirika”.

Mlipuko huo unaaminika ulitokea kwenye makutano nje ya duka Kuu la Choitram lililo na shughuli nyingi katika eneo la Wellington mjini siku ya Ijumaa.

Inasemekana wengi ya wale waliouawa katika ajali hiyo walikuwa wamekusanyika kuchota mafuta ya petroli kabla mlipuko huo kutokea.

Brima Bureh Sesay, mkuu wa Shirika la Kitaifa la Kukabiliana na Majanga la Sierre Leone, ameviambia vyombo vya habari kuwa “tuna majeruhi wengi,watu wengi wamepoteza maisha,hii ni ajali, ajali mbaya sana.”

Kulingana na mashuhuda, ajali ilitokea baada ya gari kuwaka moto katika kituo cha mafuta baada ya ajali kufanyika. Moto huo ulisambaa kwa haraka ukichoma wat una magari yaliyokuwa karibu na hapo.

Makamu wa Rais Mohammed Jurde Jaro aliwasili eneo la tukio Jumamosi baada ya kuwa nchini Scotland alikokuwa akihudhuria Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi.

Mkasa kama huu umetokea nchini Tanzania mwaka wa 2019 ambapo watu 85 waliuawa. Katika Jamhuri ya Kideokrasia ya Congo watu 50 waliuawa katika mkasa wa moto kama huo mwaka wa 2018, nchini Kenya mwaka wa 2009 takriban watu 113 waliuawa  na wengine 200 kujeruhiwa baada ya lori la mafuta kuanguka na kuwaka moto katika eneo la Sachangwan kaunti ya Molo.

.