Katika muda wa chini ya miezi 3 mzozo nchini Sudan umewalazimu karibu watu milioni 3 kukimbia makazi yao, karibu 700,000 kati yao wameondoka nchini, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) lilisema Alhamisi.
“Takriban watu milioni 3 wamekimbia makazi yao ndani na nje ya mipaka kutokana na mzozo wa Sudan, katika kipindi cha chini ya miezi mitatu. Mbali na wakimbizi wa ndani zaidi ya milioni 2.2 (IDPs), karibu wengine 700,000 wamekimbilia nchi jirani,” taarifa iliyosomwa.
Watu wengi walikwenda Misri (40%), wengine walikimbilia Chad, Sudan Kusini, Ethiopia na Jamhuri ya Afrika ya Kati, IOM inaongeza katika taarifa hiyo.
Shirika hilo linasisitiza kuwa karibu nusu ya wakazi wa nchi hiyo, au watu milioni 24.7, wanahitaji misaada ya kibinadamu na ulinzi wa dharura.
Mapigano kati ya jeshi la Sudan na waasi wa Rapid Support Forces yalizuka katikati ya mwezi Aprili. Hali bado si shwari nchini humo, licha ya mazungumzo kati ya pande hizo mbili mjini Jeddah, Saudi Arabia, yaliyoanza Mei 6.