TANZANIA: Idadi ya watu imepanuka na kufikia milioni 16 katika muongo mmoja- Rais Samia

Rais wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan amezindua matokeo ya Sensa ya Watu Nyumba na Makazi hii leo jijini Dodoma, mara ya mwisho Sensa ilifanyika mwaka 2012 chini ya awamu ya nne ya Jakaya Kikwete.

Sensa mwaka huu ilifanyika mwezi wa nane huku ikiwa na matangazo mengi na hamasa za kutosha ukilinganisha na Sensa zilizopita.

Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ambaye ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Sensa mwaka 2022 amesema, Sensa ya mwaka huu ilijawa na hamasa nyingi huku matumizi ya teknolojia yakichochea zoezi hilo kukamilika vizuri.

Naye Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi amesema Sensa ya mwaka huu imekuwa bora na yenye kukubalika Kimataifa.

Hatimaye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu akatangaza matokeo ya Sensa ya mwaka 2022, jumla ya watu wote Tanzania ni 61,741,120 kati ya hao watu 59,851,357 wapo Tanzania bara na watu 1,889,773 wapo Zanzibar.

Rais Samia amesema idadi ya Wanawake ni 31,687,990 sawa na 51% na idadi ya  Wanaume ni 30,053,130 sawa na 49% ya Watanzania wote na kubainisha kuwa idadi ya watu wa Tanzania bara imeongezeka kwa 3.2% huku upande wa Zanzibar wakiongezeka kwa 3.7%, Sensa ya mwaka huu wa 2022 imeongezeka kwa idadi ya watu milioni 16.8.

Rais Samia pia ametoa matokeo ya Sensa kwa ngazi ya Mikoa huku Mkoa wa Dar es salaam ukiwa umeongoza kwa idadi ya watu 5,383,728, ikifuatiwa na Mwanza wenye watu 3,699,872.

Kwa upande wa Zanzibar mkoa wa Mjini Magharibi ukiongoza kwa idadi kubwa ukifuatiwa na Kaskazini Pemba.

Rais Samia ametoa takwimu za majengo na matokeo yanaonyesha Tanzania ina jumla ya majengo 14,348,372 kati ya majengo hayo Tanzania bara ina majengo 13,907951 huku upande wa Zanzibar ukiwa na majengo 440.421. Pia kwa upande wa huduma za jamii kama vile vituo vya kutolea huduma za afya vipo 10,067 ambazo Zahanati zipo 7,889, vituo vya afya ni 1,490 na Hospitali zipo 688.
Kwa upande wa elimu matokeo yanaonyesha Tanzania ina jumla ya Shule 25,626 huku Shule za msingi zikiwa 19,769 na Shule za Sekondari zikiwa 5,857.