Thomas Sankara ni mmoja tu wa viongozi wa Afrika waliouwawa madarakani,fahamu wengine

Thomas Sankara, rais wa zamani wa Burkina Faso.

Kesi ya wanaume 14 akiwemo rais wa zamani wa Burkina Faso,Blaise Campaore wanaotuhumiwa kwa mauaji ya Rais Thomas Sankara miaka 34 iliyopita, imeendelea katika mahakama ya kijeshi mjini Ouagadougou Jumatatu 25 Oktoba. Kuuawa kwa Sankara,kwa miaka mingi kumeongeza machafuko na umwagaji damu katika taifa hilo.

Thomas Sankara na watu wengine 12 walipigwa risasi na kikosi cha washambuliaji Oktoba 15 1987, mauaji ya Sankara yalimleta uongozini Blaise Campaore.

Kesi kuhusu mauji ya Thomas Sankara ilianza Oktoba 11 2021, watuhumiwa 12 kati ya 14 wa mauji ya Sankara walikuwa mahakamani Jumatatu ikiwemo jenerali Gilbert Diendere aliyekuwa mkuu wa jeshi wakati wa mapinduzi ya 1987.

Bara la Afrika limeshuhudia mauaji ya viongozi tofauti kabla ukoloni na hata baada ya ukoloni kusitishwa. Baadhi ya viongozi waliouawa madarakani ni wale ambao pia waliongoza mapinduzi nchini mwao.

Thomas Sankara alikuwa afisa wa jeshi kabla kuteuliwa kuwa Waziri mkuu na baadae kiongozi wa nchi baada ya mapinduzi ya serikali. Sankara (33) alikuwa rais wa Burkina Faso taifa lililojulikana kama Upper volta hapo awali.

Thomas Sankara hufananishwa sana na kiongozi wa mapinduzi kutoka Cuba Che Guevara na alifanya mageuzi mengi ya serikali kama alivyofanya kiongozi huyo wa Cuba. Tarehe 15 Oktoba 1987, Sankara aliuliwa katika mapinduzi ya serikali yanayodaiwa kuongozwa na Blaise Campaore.

Blaise Campaore, Rais wa zamani wa Burkina Faso.

Melchior Ndadaye alikuwa rais wa kwanza wa Burundi kutoka jamii ya Hutu. Ndadaye alishinda uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia nchini humo wa mwaka 1993. Juhudi zake za kutaka kukomesha uhasama kati ya jamii za Hutu na Tusti ziliambulia patupu wakati jeshi lililokuwa na wingi wa waTutsi kufanya mapinduzi ya serikali,na miezi mitatu baada ya kuchukua uongozi wa nchi, Melchior Ndadaye aliuliwa kwenye majaribio ya mapinduzi Oktoba 21 1993.

Taifa la kaskazini mwa Afrika la Chad, limekumbwa na misukosuko ya kisiasa katika miaka ya hivi karibuni. Mapema mwaka huu aliyekuwa Rais wa Chad Idriss Deby, aliyekuwa ameongoza taifa hilo kwa zaidi ya miongo mitatu aliuliwa kwa kupigwa risasi alipokuwa mstari wa mbele katika vita na wanamgambo katika mpaka wa kasakzini nchi humo.Mtoto wake Mahamat Idriss Déby Itno amechukua uongozi wa nchi.

Idriss Deby, Rais wa zamani wa Chad

Rais wa kwanza wa Chad Francois Tombalbaye, alikuja uongozini 11 Agosti 1960. Alitawala kwa udikteta hadi mwaka wa 1975 na kuuawa na majeshi ya Chad.

Patrice Lumumba alikuwa Waziri mkuu wa kwanza baada ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kupata uhuru.

Punde tu baada ya kupatikana kwa uhuru, maasi yalizuka katika jeshi, Lumumba alitafuta usaidizi kutoka Marekani na Umoja wa Mataifa, alipokosa usaidizi aligeukia Usovieti.Hatua ya kugeukia Usovieti ilionekana kama uasi na ukachangia uhasama dhidi yake kutoka kwa Umoja wa Mataifa, Rais wakati huo Joseph Kasa-Vubu na kiongozi wa wafanyakazi Joseph – Desire Mobutu pamoja na Marekani na Ubelgiji.

Lumumba alijaribu kutoroka baada ya Mobutu kuongoza mapinduzi, alikamatwa na kuuliwa kwa kupigwa risasi hadi kufa mnamo Januari 17 1961.

Patrice Lumumba, waziri mkuu wa zamani DRC

Laurent Kabila alikuwa rais wa tatu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo baada ya kumpindua rais wa pili Mobutu Sese Seko. Kabila aliuliwa Januari 16 2001.

Mohamed Anwar El Sadat alikuwa rais wa tatu wa Misri, akiwa afisa wa jeshi la Free Officers walimpindua Mfalme Farouk uongozini mwaka wa 1952. Juhudi zake za kuleta amani kati ya Misri na Israel zilimshindia tuzo ya Amani ya Nobel na akawa muislamu wa kwaza kushinda tuzo hiyo.

Mgogoro uliokuwa kati ya mataifa ya kiarabu na Misri kuhusu kupatikana kwa amani kati ya Misri na Israel kulichangia mauaji yake mnamo mwaka wa 1981 alipopigwa risasi na wapiganaji katika gwaride mjini Cairo na kuawa.

Joao Bernardo Vieira alikuwa rais wa Guinea Bissau kati ya 1980 na 1999 na tena kati ya 2005 hadi 2009. Vieira alikuja uongozini baada ya kuipindua serikali ya Rais Luis Cabral mwaka wa 1980. Baada ya kurudishwa kwa mfumo wa vyama vingi, Vieira alishinda uchaguzi na kuongoza kati ya 1994 hadi 1998 alipofurushwa na akaenda uhamishoni baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kuzuka nchini humo. Alirudi nchini mwaka wa 2005 na akashinda uchaguzi wa mwaka huo.

Joao Vieira alipigwa risasi na majeshi mnamo Machi 2 2009 katika kitendo cha kulipiza kisasi baada ya shambulio la bomu kumuua Jenerali wa majeshi Batista Tagme Na Waie.

Viongozi wengine kutoka bara Afrika ambao waliuliwa ni pamoja na marais wa zamani wa Liberia, William.R. Tolbert mwaka wa 1980 na Samuel Doe mnamo Septemba 9 1990.

Samuel Doe alikuwa rais wa 21 wa Liberia aliyeingia uongozini baada ya kufanya mapinduzi makali ya serikali mwaka wa 1980 alipokuwa sajenti mkuu katika kikosi cha majeshi.Katika mapinduzi aliyekuwa rais wakati huo William Tolbert na wanachama wengine wa True Whig Party waliuliwa.

Samuel Doe,rais wa 21 wa Liberia

Rais wa zamani wa Libya, Muammar Gaddafi aliuliwa mwaka wa 2011 baada ya kuongoza nchi kati ya 1969 hadi 2011.

Rais wa Rwanda Juvenal Habyarimana alikuwa rais wa pili wa Rwanda aliyehudumu kati ya 1973 hadi 1994. Habyarimana aliingia uongozini baada ya kupindua serikali ya rais wa kwanza Gregoire Kayibanda mwaka wa 1973.

Mnamo mwaka wa 1990, jeshi lililoongozwa na waTutsi la Rwanda Patriotic Front lilizindua mapigano ya wenyewe kwa wenyewe dhidi ya serikali ya Habyarimana. Na mwaka uliofuatia ndege aliyokuwa ameabiri akiwa na rais wa Burundi Cyprien Ntaryamira ilitunguliwa karibu na Kigali viongozi hao wawili waliuawa katika kisa hicho.

Mauaji yake yalisababisha mauaji ya halaiki nchini humo.

Kusikizwa kwa kesi ya Thomas Sankara miaka 34 baada ya mauaji yake kunawapa wananchi matumaini ya haki kutendeka katika mataifa yao pia.

Juvenal Habyarimana Rais wa zamani wa Rwanda