Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC) wamesema kutowasikiliza Wamaasai wanaioshi katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ni kuwanyima haki zao.
Kauli hiyo inakuja wakati mamia ya vijana na wakina mama wa eneo hilo walipoandamana jana wakiishinikiza Serikali kuwapa huduma za mbalimbali za kijamii.
Akizungumza jana, Katibu wa TEC Padri Charles Kitima alisema kutowasikiliza wamasai wa Hifadhi ya Ngorongoro ni kuwanyima haki zao
Hapo jana inaelezwa kuwa maandamano ya amani yaliyofanywa na jamii ya wamasaai yalidumu kwa takribani saa nne huku shughuli za utalii zikilazimika kusimama.
Watetezi wa haki za binadamu nchini Tanzania pia wamezitaka mamlaka za Tanzania kuheshimu haki za jamii hiyo kwa kusikiliza na kuwapa mahitaji yao ya msingi.
Hayo yakijiri ni kwamba Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika(TLS), wakili Boniface Mwabukusi amesema TLS itaungana na yeyote kuhakikisha haki za Wamaasai wa Ngorongoro zinapatikana hasa kwenye mchakato wa kupiga kura na kuchagua viongozi wao.
Pamoja na hayo pia amesema TLS haitasita kuchukua hatua ikiwemo ya msaada wa kisheria kwa wale wote waliofanyiwa dhuluma ya demokrasia akitolea mfano kilichotokea jijini Mbeya na kwamba tayari mchakato umeanza kuwasaidia wahanga katika tukio lile.
Tangu mwaka 2022, Mamlaka nchini Tanzania zimekuwa zikiendesha zoezi la kuhamisha watu kutoka eneo hilo la hifadhi kwenda kwenye eneo la Msomera mkoani Tanga.
Hata hivyo, tangu kuanza kwa zoezi hilo takribani watu 7,000 wameshahama kwa hiari huku baadhi wakieleza kutokuwa tayari kuhama.