Serikali ya Togo imepiga marufuku maandamano ya upinzani yaliyopangwa kufanyika Jumamosi huko Lome, ikitoa sababu za ‘usalama,’ kulingana na taarifa rasmi.
Dynamique Monseigneur Kpodzro, au muungano wa DMK, ambao unajumuisha vyama saba na mashirika kadhaa ya kiraia, ulikuwa umepanga maandamano kupinga gharama ya maisha, utawala mbaya na ukosefu wa haki.
Mikutano ya upinzani ni nadra nchini Togo ambako wakosoaji wanasema wapinzani wamezimwa chini ya Rais Faure Gnassingbe, ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 17.
“Mpangilio wa mkutano huo katika mazingira ya sasa ya usalama wa kikanda na kitaifa unaleta wasiwasi,” Waziri wa Usalama, Jenerali Yark Damehame, alisema katika taarifa yake Jumatano.
Ilisema maandamano hayo “yana uwezekano wa kuathiri juhudi za kuhifadhi utulivu na usalama wa umma.”
Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa mamlaka kupiga marufuku mkutano wa hivi majuzi wa upinzani kwa sababu za kiusalama.
Katika kilele cha janga la UVIKO 19, maafisa walisimamisha mikusanyiko ya upinzani juu ya hatari za kiafya.
“Uamuzi huu haukubaliki. Katika nchi kama Mali ambako hatari ya usalama iko juu sana, idadi ya watu bado wanatumia haki zao kama raia,”mratibu wa DMK Brigitte Kafui Adjamagbo-Johnson aliiambia AFP.
Kaskazini mwa Togo imekumbwa na mashambulizi mawili ya wanajihadi mwaka huu, ikiwa ni mara ya kwanza tangu jeshi liimarishe vikosi vyake katika eneo hilo kukabiliana na tishio kutoka kwa wanamgambo katika mpaka wa Burkina Faso.
Wanajeshi wanane waliuawa katika moja ya mashambulizi ambayo yalidaiwa na muungano wenye makao yake nchini Mali wa wanajihadi wenye mafungamano na wanajihadi Jama’at Nasr al-Islam wal Muslimin, au JNIM.
Mapema mwezi huu, Togo ilitangaza hali ya hatari katika majimbo yake ya kaskazini.
DMK ni vuguvugu lililomuunga mkono waziri mkuu wa zamani Agbeyome Kodjo, ambaye aliibuka wa pili katika uchaguzi wa urais wa 2020 kwa asilimia 19.46 ya kura dhidi ya asilimia 70.78 ya Gnassingbe.
Kwa sasa yuko uhamishoni, Kodjo bado anapinga matokeo ya uchaguzi katika jumbe zinazotangazwa kwenye mitandao ya kijamii.
Gnassingbe aliingia madarakani mwaka wa 2005 baada ya kifo cha babake, Jenerali Gnassingbe Eyadema, ambaye alikuwa ametawala Togo kwa miaka 38.
Alichaguliwa tena katika kura ambazo zote zilipingwa na upinzani.