Msumbiji siku ya Jumatatu ilisema mfumo wa mtandao unaotumiwa na tovuti za serikali ulidukuliwa na kuilazimisha kuondoa tovuti zote za serikali kwa saa kadhaa.
Alielezea shambulio hilo kama “aina ya uharibifu wa wavuti” na tovuti ya habari inayoendeshwa na watu binafsi, Carta de Mozambique, ilisema kurasa za wavuti za serikali zimebadilishwa na kuwekwa picha zinazohusiana na wanajihadi.
“Mitandao ambayo huchapisha habari kwa matumizi ya umma ilishambuliwa,” afisa mkuu wa serikali anayehusika na mifumo ya mawasiliano ya kielektroniki Herminio Jasse, aliwaambia waandishi wa habari.
“Baada ya shambulio hilo tulizima sava mara moja. Hii ilizua wasiwasi kutoka kwa watu wanaojaribu kufikia tovuti,” alisema.
Mkoa wa kaskazini wa Cabo Delgado nchini Msumbiji umekumbwa na ghasia mbaya zinazoendeshwa na wanamgambo wanaohusishwa na kikundi kinachojiita Islamic State.
Kundi hilo la itikadi kali limeshambulia miji na vijiji kaskazini mwa Msumbiji tangu mwaka 2017 kwa lengo la kuanzisha ukhalifa wenye misimamo mikali.
Machafuko hayo yamegharimu maisha ya zaidi ya watu 3,700 na kuwafanya karibu watu 800,000 kuyahama makazi yao.
Tangu Julai zaidi ya wanajeshi 3,100 wametumwa kutoka Rwanda na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika yenye nchi 16 kusaidia jeshi la Msumbiji kuwaondoa wapiganaji hao.
Kutumwa kwa wanajeshi wa kigeni kumesaidia kukomesha ghasia hizo, kwa mujibu wa taasisi ya kimataifa ya International Crisis Group