Mtangazaji wa kipindi cha ‘The Daily Show’ Trevor Noah ataondoka katika kipindi cha vichekesho cha kejeli baada ya miaka saba, alisema Alhamisi Septemba 29, bila kutoa ratiba ya kuondoka kwake.
“Muda wangu umekwisha,” mchekeshaji huyo mwenye umri wa miaka 38 alisema katika video kwenye akaunti ya Twitter ya kipindi hicho.
Mchekeshaji huyo wa Afrika Kusini amesema alikosa kusafiri baada ya kuzuiwa na janga la Covid-19. “Nilikaa miaka miwili katika nyumba yangu, sio barabarani,” alisema. “Niligundua kuna sehemu nyingine ya maisha yangu ambayo ninataka kuendelea kuchunguza.”
Kipindi hicho kilipata umaarufu chini ya mtangazaji wa zamani Jon Stewart, ambaye alikuwa mwenyeji wa kipindi hicho kwa miaka 16 kabla ya kuondoka mwaka 2015. Ilikuja kama mshangao kwa wengi wakati Noah, ambaye hakujulikana, alipotangazwa kama mbadala wa Stewart.
Hakujakuwa na dalili za ni nani atakayechukua madaraka kutoka kwa Noah. “Bila ratiba ya kuondoka kwake, tunafanya kazi pamoja katika hatua zinazofuata,” Paramount Global cable network ulisema, ambao unamiliki kipindi cha Comedy Central, katika taarifa kwa vyombo vya habari vya Marekani.
Noah alielezea malezi yake katika enzi ya ubaguzi wa rangi Afrika Kusini kama mtoto wa mama mweusi wa Afrika Kusini na baba mzungu wa Uswisi na Ujerumani katika “Born a Crime”, kumbukumbu yake iliyouzwa zaidi mwaka 2016.
“Nimependa kuandaa kipindi hiki, imekuwa moja ya changamoto zangu kubwa na moja ya furaha yangu kubwa,” alisema Noah.