Trump aapishwa kuwa Rais wa Marekani tena

Rais Donald Trump aliahidi “enzi za dhahabu” kwa Marekani alipokuwa akiapishwa kwa muhula wake wa pili kama Rais wa Marekani, siku ya Jumatatu Januari 20, lakini aliweka mkazo kwenye sera kali za kubadili kile alichokiita “anguko la Marekani.”

Katika hotuba yake ya kipekee, Trump alizungumzia masuala kama uhamiaji haramu na vita vya tamaduni, akisema kuwa “enzi za dhahabu za Marekani zinanza sasa.” Aliongeza kwa kusema, “Kuanzia leo, nchi yetu itastawi na kuheshimiwa tena duniani kote.”

Trump pia alizungumzia kushindwa kwa serikali ya Rais Joe Biden na kusema “anguko la Marekani limeisha.” Alisema kuwa atapigania haki ya Amerika na kuanzisha amri za utendaji, akisisitiza kuhusu sera za kupambana na uhamiaji haramu na kuhamasisha “vita vya biashara.”

Trump alitangaza kuwa serikali yake itakubali jinsia mbili pekee: kiume na kike, na kumaliza utaratibu wa kutambua jinsia ya tatu kwenye baadhi ya nyaraka rasmi.

Rais Trump pia aliahidi kutoka kwenye makubaliano ya mabadiliko ya tabianchi ya Paris na kutangaza vita dhidi ya sera za utofauti na usawa.

Kwa upande wa dunia, Trump alikaribishwa na viongozi wa dunia kama Rais Vladimir Putin wa Urusi na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu wa Israel, ambao walimpongeza kwa kurudi madarakani.