Tume ya ukweli na maridhiano ya Gambia imempata Rais wa zamani Yahya Jammeh kuhusika na mfululizo wa mauaji, ubakaji na mateso wakati wa utawala wake wa kidikteta uliodumu kwa miaka 22 na kupendekeza ahukumiwe mbele ya mahakama ya kimataifa.
“Katika kipindi cha miaka 22, kuanzia Julai 22, 1994, Yahya Jammeh na wahusika wenza walifanya uhalifu mkubwa sana dhidi ya watu wa Gambia,” taarifa ya tume hiyo ilisema.
Tume hiyo ilisema kuwa Jammeh na waandamizi wake, ikiwa ni pamoja na kikosi cha wapiganaji kiitwacho The Junglas, walihusika na uhalifu mahususi 44 dhidi ya waandishi wa habari, wanajeshi wa zamani, wapinzani wa kisiasa na raia.
Tume hiyo ilipendekeza “kuwa Yahya Jammeh na wahusika wenzake wafunguliwe mashtaka katika mahakama ya kimataifa” huko Afrika Magharibi nje ya Gambia, chini ya Umoja wa Afrika au kundi la kikanda la ECOWAS, taarifa hiyo iliongeza.