Tundu Lissu: hakuna uchaguzi Tanzania bila ya mageuzi kwenye tume ya Uchaguzi

Mwenyekiti mpya wa Chama Kikuu cha Upinzani nchini Tanzania, CHADEMA, Tundu Lissu amesema chama hicho hakitasusia uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

 

Amesema badala yake kitahakikisha uchaguzi huo hautafanyika endapo hakutakuwa na mageuzi wanayoyashinikiza kwenye mfumo wa uchaguzi.

Akizungumza na waandishi habari mjini Dar es Salaam, Lissu amesema CHADEMA kitaishtaki serikali ya Tanzania kwa wananchi, jumuiya ya kimataifa na viongozi wa kidini ili kushinikiza mabadiliko ya katiba na sheria za uchaguzi alizosema kila wakati zinachangia kufanyika uchaguzi usiozingatia misingi ya demokrasia.

Amesema mfumo huo wa uchaguzi umesababisha Tanzania kuongozwa na viongozi ambao hawakuchaguliwa kwa njia halali miaka ya hivi karibuni.

“Tunaposema bila Mabadiliko ya mfumo hakuna Uchaguzi tunaamnisha kwamba hatutasusia Uchaguzi ila tutafanya kila lililo ndani ya uwezo wetu kwa nguvu tulizonazo kuhakikisha Uchaguzi haufanyiki”. Mhe. Tundu Lissu Mwenyekiti wa Chadema Taifa.

Pia ametaka mageuzi kabambe ndani ya tume ya taifa ya uchaguzi kabla ya uchagzui mkuu wa mwaka huu wa 2025.

‘’Mfumo wetu wa uchaguzi unahitaji mageuzi. Kuanzaia kwa mwenyekiti wa uchagzui, makamishna hadi kwa wasaidizi wa uchaguzi, wote ni wateule wa rais. Na pia rais anaweza wafuta kazi wakati wowote. Kwa hivyo, tukielekea uchaguzini na huu mfumo, tutakatwa wote’’ alisema Lissu

Aidha, Lissu amekosoa mfumo wa ugavi wa majimbo katika muungano wa jamhuri ya Tanzania. Ametaka majimbo yagawanywe kulingana na idadi ya watu.

‘’ kulingana na takwimu ya tume ya taifa ya uchaguzi yam waka wa 2020, Zanzibar mzima ilikuwa na idadi ya wapiga kura 566,917 na ikatengewa majimbo 50 ilhali mkoa wa Dar es Salaam ina idadi ya wapiga kura 3,427, 353 na ikatengewa majimbo 10. Na ukijumlisha Mikoa ya Dar es Salaam, Tabora, Mwanza, Morogoro na Kagera, idadi ya wapiga kura ni takiribani milioni 9.3. na kutengewa majibo 51. Alitangaza Lissu.

Lissu amewasihi mashirika ya kijamii, vyama vingine vya kisiasa, viongozi wa dini, jumuiya ya kimataifa na watanzania wenye mapenzi mema kujumuisha nguvu ili kutafuta haki ya mfumo ya uchaguzi nchini Tanzania.

“Mapambano haya yatahitaji baraka za kila mmoja wetu, yatahitaji kila mmoja wetu kuweka mkono wake, kila mmoja kuweka kidogo alichonacho, jambo likapata baraka za wengi linapata baraka za Mungu. Hii kazi itahitaji kujitolea sana, itahitaji twende kila mahali kwenye nchi yetu kufanya mikutano ya haghara na ya ndani. Kwa yeyote anayetaka kuweka mkono wake wa baraka katika hizi harakati za kudai haki katika nchi yetu achangie” Mhe. Tundu Lissu

Tundu Lissu alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa chama hicho Januari 22 2025, na kumshinda aliyekuwa mwenyekiti Freeman Mbowe.