Makamu mwenyekiti wa Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, CHADEMA Tundu Lissu amedai kuwa ‘watu wasiojulikana’ wanapanga kumdhuru wakati ambapo chama hicho kinakaribia kufanya uchaguzi wa vyeo mbali mbali ya juu ya chama ikiwemo ya mwenyekiti ambayo ametangaza kuwa anawania.
Katika chapisho kwenye mtandao wake wa X , Lissu amesema kwamba ‘watu wasiojulikana’ wanapanga kumdhuru halafu badala yake wamsingizie mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe kuwa ndiye aliyetekeleza shambulio dhidi yake.
Amesema kwamba watu hao wamekuwa wakitekeleza mauaji kwa watu wasio na hatia kisha, wanasingizia watu wengine ili waliohusika wasiwajibike na udhalimu walioufanya.
‘’Enyi watu wabaya mjulikanao kama watu wasiojulikana, nimezisikia njama zenu. Mnataka kuniumiza halafu mumsingizie Mwenyekiti wetu wa chama,’’ aliandika Tundu Lissu.
CHADEMA inaelekea kwenye kilele cha uchaguzi wa ndani wa chama hicho huku Lissu akichukua rasmi cheti cha kuwania nafasi ya uenyekiti. Lissu atamenyana Freeman Mbowe kwenye nafasi ya juu zaidi ya chama hicho.
Tangazo la Lissu limezua gumzo na hata nyufa baina ya wafuasi wa kambi za Lissu na Mbowe.
‘’Ndivyo mlivyofanya wakati wa kifo cha marehemu Chacha Wangwe. Ndivyo mlivyofanya tena wakati mliponishambulia tarehe 7 Septemba 2017 na ndivyo mlivyofanya miezi michache iliopita mlipomteka nyara na kumuua Mzee Ali Mohamed kibao‘’, alisema Tundu Lissu katika chapisho hilo la mtandao wa X
Mwaka 2017, Lissu alishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana nje ya makazi yake mjini Dodoma alipokuwa akihudhuria vikao vya Bunge.
Lissu alilizimika kukimbizwa Nairobi, Kenya na baadae Ubelgiji kwa matibabu. Lissu amesalia na ulemavu wa kudumu kutokana na shambulio hilo.
Hakuna mtu aliyekamatwa wala kufunguliwa mashtaka kutokana na shambulio hilo huku Lissu mwenyewe akiilaumu serikali ya utawala wa hayati John Magufuli kwa kutekeleza shambulio hilo, tuhuma ambazo serikali ya Tanzania imezikanusha.