Idadi ya wahamiaji waliouawa baada ya boti zao kuzama mwishoni mwa mwezi uliopita wakati wa jitihada za kuondoka Tunisia kuelekea Ulaya imeongezeka hadi 24, chanzo cha mahakama kilisema Jumatano.
Boti nne zilipinduka nje ya ufuo wa mji wa bandari wa kati wa Tunisia wa Sfax usiku wa Aprili 22-23.
Huku watu 97 wakiokolewa, 24 sasa wamepatikana wakiwa wamekufa, wakiwemo wanawake na watoto, alisema msemaji wa mahakama ya Sfax Mourad Turki.
Mamlaka hapo awali ilisema walikuwa wameopoa miili 17.
Chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Sfax, katika eneo hilo kilipokea miili ya wahamiaji,chumba hicho kimepokea maiti 92 za aina hiyo katika miezi ya hivi karibuni, wengi wao wakiwa watu kutoka Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Tunisia inajitahidi kukabiliana na kuongezeka kwa wahamiaji kwani ‘hakuna nafasi iliyobaki’ katika makaburi ya karibu ya wahamiaji, Turki alisema.
Aliongeza kuwa karibu miili 40 ilikuwa imelazwa kwenye sakafu kwa kukosa nafasi.
Manispaa nyingi za Tunisia zinakataa kuchukua jukumu la kutunza maiti za wahamiaji haramu.
Tunisia imekuwa njia kuu kwa wahamiaji wanaojaribu kufika Ulaya kupitia njia hatari zaidi ya uhamiaji duniani, katikati mwa Mediterania.
Takriban wahamiaji 2,000 walitoweka au kufariki katika bahari ya Mediterania mwaka jana, kutoka 1,400 mwaka uliopita, kulingana na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji.