Milki za Kiarabu imetangaza Jumanne kwamba wiki ya kazi itakuwa siku nne na nusu, ikiwa ni Ijumaa alasiri, Jumamosi, na Jumapili kuunda wikendi mpya. Idara zote za serikali ya Shirikisho zitahamia kwa wikendi hii mpya kuanzia Januari 1, 2022.
Mamlaka iliongeza kuwa kutokana na hatua hii UAE imekuwa taifa la kwanza duniani kuanzisha wiki ya kazi iliyo fupi kuliko wiki ya kawaida ya siku tano kama ilivyo kwa mataifa mengine.
Wiki ya kazi itaanza Jumatatu na kumalizika Ijumaa alasiri. Saa za kazi kwa wafanyakazi wa shirikisho zitaanza saa 1:30 hadi saa 9:30, ikiwa ni jumla ya saa 8.5 za kazi kwa siku. Siku ya Ijumaa, wafanyikazi watafanya kazi kwa saa 4.5 pekee.
Siku ya Ijumaa, wafanyakazi pia wataruhusiwa kuchagua iwapo watafanya kazi kutoka nyumbani au ofisini. Kulingana na serikali ya shirikisho, wikendi ndefu inalenga kuongeza tija na kuboresha usawa wa maisha ya familia na kufikia kiwango kikubwa cha utendaji wa kukuza uchumi wa nchi.