Polisi nchini Uganda siku ya Jumatatu waliwarushia gesi ya kutoa machozi waandamanaji waliokuwa wakiandamana kuhusu kupanda kwa bei ya mafuta na vyakula vya msingi, huku watu kadhaa wakikamatwa, polisi na mashahidi walisema.
Ilikuwa ni mara ya pili katika mwezi mmoja ambapo waandamanaji wamejitokeza barabarani kuelezea hasira zao juu ya kupanda kwa gharama ya maisha katika nchi ambayo uchumi wake umeathiriwa sana na janga la Covid-19 na hivi karibuni vita vya Ukraine.
Huko Jinja, mji wa viwanda ulio kando ya Ziwa Victoria kusini mashariki mwa Uganda, waandamanaji walichoma moto matairi na kufunga barabara kabla ya polisi kuwatawanya kwa mabomu ya machozi, walioshuhudia walisema.
Matukio kama hayo yalishuhudiwa katika miji ya Kamuli na Luuka kaskazini mwa Jinja, walisema.
Msemaji wa polisi wa Uganda Fred Enanga aliwaambia waandishi wa habari katika mji mkuu Kampala kwamba maandamano hayo yalizimwa.
Watu kadhaa wamekamatwa na watashtakiwa alisema, bila kutoa maelezo zaidi.
Alidai waandamanaji “wanataka kutumia hofu kuendeleza vurugu, na itasababisha ukosefu wa usalama nchini kote ikiwa hautakomeshwa.”
Muuza matunda Moses Lukwanga, 59, alisema kwamba waandamanaji huko Jinja walichoma matairi na kuweka vizuizi kuzuia kukabiliwa na polisi.
“Waandamanaji waliwalazimisha watu kufunga biashara na wakati polisi walikuja kuwatawanya kwa mabomu ya machozi, mtaa mzima ulikuwa hauna watu.”
Richard Mukose, dereva wa teksi mwenye umri wa miaka 35 kutoka Kamuli, alisema sehemu ya barabara inayounganisha mji huo na Jinja ilifungwa na waandamanaji kabla ya polisi kufyatua vitoza machozi na kuwaondoa eneo hilo.
Mjini Kampala, trafiki na biashara ziliendelea kama kawaida, lakini kulikuwa na msururu mkubwa wa polisi wakiungwa mkono na wanajeshi.
Kwa wiki moja, jumbe zimekuwa zikisambazwa kwenye mitandao ya kijamii zikiwataka raia wa Uganda kusalia majumbani mwao na kuacha kulipa ushuru ili kushinikiza serikali kuchukua hatua kutokana na kupanda kwa bei ya bidhaa.
Lakini Rais Yoweri Museveni amesema kuwa kupunguzwa kwa kodi au kuunda ruzuku kujaribu kutatua mzozo huo kungefanya hali kuwa mbaya zaidi kwa kuwapa watu ‘faraja ya bandia.’