Polisi wa Uganda walifyatua gesi ya kutoa machozi na kuwakamata takriban waandamanaji kumi na wawili siku ya Jumatatu baada ya maandamano ya kupinga ongezeko kubwa la bei ya vyakula na mafuta katika taifa hilo.
Uganda ni nchi ya watu milioni 45 na inakabiliwa na mdororo wa kiuchumi uliochochewa na janga la UVIKO 19 na vita vya Urusi nchini Ukraine.
Mfumuko wa bei za vyakula uliongezeka zaidi ya mara mbili hadi asilimia 13.1 mwezi Mei, kulingana na takwimu za hivi punde za serikali.
Siku ya Jumatatu, waandamanaji walichoma matairi yaliyotumika kufunga barabara kuu yenye shughuli nyingi huko Jinja, yapata kilomita 80 mashariki mwa mji mkuu Kampala, wakiitaka serikali kutoa ruzuku ya chakula.
“Polisi walitumia nguvu kidogo ikiwa ni pamoja na vitoa machozi kuwatawanya waandamanaji,”msemaji wa polisi wa eneo hilo James Mubi alisema.
“Viongozi wanane kati ya viongozi hao walikamatwa,”alisema na kuongeza kuwa watashtakiwa Jumanne kwa kuchochea ghasia.
Waandamanaji hao waliwalazimisha madereva wa magari kuungana nao ili kuitisha mabadiliko, walioshuhudia walisema.
“Tunaunga mkono maandamano kama haya. Serikali lazima ichukue hatua. Watu wanalala njaa,” mfanyabiashara wa vipuri mwenye umri wa miaka 28 Solomon Wandibwa alisema.
Bei za mafuta, vyakula na bidhaa nyingine za kimsingi zimepanda kwa kasi duniani kote kutokana na vita vya Ukraine, na kukumba zaidi nchi za Afrika na kwingineko.
Nchini Uganda, petroli inauzwa kwa shilingi 7,000 (dola 1.85) kwa lita, ongezeko la mara mbili tangu Februari.
Katika baadhi ya maeneo ya vijijini, vituo vya mafuta vinauza lita moja ya mafuta hadi shilingi 10,000.
Huku hali ya kutoridhika ikiendelea kuongezeka kutokana na kupanda kwa bei, Rais Yoweri Museveni amepuuza mara kwa mara wito wa kupunguzwa kwa ushuru na ruzuku, akiwataka raia badala yake kupunguza mahitaji yao.
Katika hotuba yake ya kila mwaka ya hali ya taifa mwezi Juni, Museveni alisema, “Kukata kodi na ruzuku, hasa kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje, ni kujitoa mhanga kwa sababu watu wetu wanaweza kununua bidhaa ovyo na hatimaye kupoteza akiba yetu ya fedha za kigeni.”
Aliyekuwa mgombea urais wa Uganda Kizza Besigye alishtakiwa mwezi uliopita kwa kuchochea ghasia kwa kuongoza maandamano ya kupinga mfumuko wa bei ambao umeikumba Uganda.