Mahakama ya Uganda Jumatatu iliamuru mwandishi mashuhuri kufikishwa mahakamani mwezi ujao kwa tuhuma za kumtusi Rais Yoweri Museveni na mwanawe.
Kakwenza Rukirabashaija alizuiliwa muda mfupi baada ya sikukuu ya Krismasi na baadaye kushtakiwa kwa “mawasiliano ya kukera” katika kesi ambayo imezua wasiwasi wa kimataifa.
Mwandishi huyo wa riwaya ya kejeli mwenye umri wa miaka 33 anasema aliteswa kizuizini na alionekana kwenye runinga mwishoni wa wiki akiwa na majeraha mgongoni mwake na makovu kwenye sehemu zingine za mwili wake.
“Walinipiga kwa fimbo, kila mahali. Unaanguka wanakupiga, unainuka, unapoteza fahamu,” alisema kwenye mahojiano na kituo cha televisheni cha NTV Uganda Jumamosi
Hakimu mkuu Douglas Singiza alitangaza tarehe ya kusikilizwa kwa kesi hiyo Machi 23 lakini alikataa kulegeza masharti ya dhamana ya Rukirabashaija yaliyowekwa katika kesi ya Januari, ambayo ni pamoja na amri ya kutozungumza na wanahabari.
Singiza alimuonya mwandishi huyo kwamba kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu kesi yake kunatoa shinikizo lisilo la lazima kwa mahakama hiyo.
Mashtaka dhidi yake yanahusiana na maoni yasiyofurahisha kwenye Twitter kuhusu Museveni, ambaye ametawala Uganda tangu 1986, na mtoto wake Muhoozi Kainerugaba.
Katika chapisho moja, alimtaja Kainerugaba, jenerali ambaye Waganda wengi wanaamini kuwa anajiweka katika nafasi ya kuchukua uongozi kutoka kwa babake mwenye umri wa miaka 77, kama “mtu mnene.”
Mateso aliyopitia
Katika mahojiano ya televisheni Jumamosi — yaliyofanywa licha ya masharti ya dhamana — mwandishi alielezea kulazimishwa kucheza bila kupumzika akiwa na wafungwa wengine.
Akielezea mbinu ambayo wapinzani wengine wa Uganda wanadai imetumiwa dhidi yao, Rukirabashaija pia alisema vifaa vya chuma vilitumika kumsababishia majeruhi. Alidai pia kwamba alidungwa sindano ya kitu kisichojulikana mara kadhaa kinyume na matakwa yake.
Uganda imeshuhudia msururu wa mikasa inayolenga kukomesha upinzani, huku waandishi wa habari wakishambuliwa, mawakili kufungwa, waangalizi wa uchaguzi kufunguliwa mashtaka na viongozi wa upinzani kunyamazishwa.
Siku ya Jumatatu, Umoja wa Ulaya na mataifa kadhaa wanachama walitoa taarifa ya pamoja wakitaka “uchunguzi wa kina” ufanywe kuhusu ukiukaji wa haki nchini Uganda.
Taarifa hiyo ilionyesha wasiwasi “kutokana na ongezeko kubwa la ripoti za utesaji, kukamatwa kiholela, kutoweka kwa nguvu, unyanyasaji pamoja na mashambulizi dhidi ya watetezi wa haki za binadamu, wanachama wa upinzani na wanaharakati wa haki za mazingira.”
Rukirabashaija alijishindia sifa kwa riwaya yake ya kejeli ya 2020 “The Greedy Barbarian” ambayo inaelezea ufisadi wa hali ya juu katika nchi ya kubuni.
Alitunukiwa Tuzo ya 2021 ya PEN Pinter kwa Mwandishi wa Kimataifa wa Ujasiri, ambayo hutolewa kila mwaka kwa mwandishi ambaye ameteswa kwa kusema juu ya imani zao.
Mnamo 2020, pia alishikiliwa kwa wiki moja baada ya kukamatwa kwa kukiuka sheria za UVIKO-19 za kutengwa kwa jamii na kuchochea ghasia.