Hofu imewakumba wananchi wa Malawi kufuatia taarifa kuwa ugonjwa hatari wa kuambukiza wa ukoma umezuka upya nchini humo. Mamlaka zimesema kuwa hadi sasa visa 150 vimeripotiwa katika miezi michache iliyopita.
Mratibu wa Mpango wa Kitaifa wa Kifua Kikuu na Ukoma Dkt. James Mpunga alitangaza hayo wakati wa mkutano wa wadau iliofanyika Dowa siku ya Jumatatu.
“Ingawaje Malawi ilifaulu kuangamiza ugonjwa huo kwa kiasi kikubwa, kuna visa vichache ambavyo bado huripotiwa katika wilaya tofauti na ni wazi kuwa ugonjwa huo bado upo nasi.” Alisema Dkt. Mpunga.
Malawi ilifikia kiwango cha kutokomeza ukoma mwaka wa 1994. Kufuatia ripoti hii mpya, mapendekezo ya serikali ni kuwa serikali iwajibike kutokomezza kabisa ukoma na kifua kikuu kufikia 2030.
Ugonjwa wa ukoma unasababishwa na bakteria aina ya mycobacterium leprae. Ugonjwa huu unaweza kukingwa na kutibiwa, ila usiposhughulikiwa mtu huanza kukatika sehemu za mwili kama vidole.
Si mara ya kwanza kwa ugonjwa huo kuripotiwa nchini Malawi. Ukoma uliaminika kutokomezwa mwaka wa 1970 na Shirika la Afya Duniani likatangaza hayo pia.
Mwaka wa 2014 visa 554 vya ukoma viliripotiwa na visa 629 kuripotiwa mwaka wa 629.
Ugonjwa wa ukoma umekuwepo kutoka enzi za biblia na ingawaje si hatari kama ulivyokuwa enzi hizo, ugonjwa huo husababishwa na bakteria na huambukiza kwa urahisi kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kupitia kupiga chafya na kukohoa.
Ugonjwa wa ukoma unaweza kutibika iwapo mtu atapata huduma za matibabu mapema. Visa vya ukoma vimepungua kutoka milioni 5,2 mwaka wa 1985 hadi visa 210,000 kwa mwaka sasa. Ukoma unapatikana katika mataifa 100 kote duniani.