Huku uhalifu wa mtandaoni ukikithiri barani Afrika, wahamasishaji kuhusu usalama wa mtandao kote barani wameungana kusaidia Waafrika kuwa salama mtandaoni kupitia elimu kwa umma.
Mtandao wa African Cybersmart ulizinduliwa wiki iliyopita jijini Nairobi, Kenya ili kuwezesha kujenga uwezo na ushirikiano kati ya wahamasishaji kuhusu usalama wa mtandao barani humo.
Uzinduzi huo ulifanyika wakati wa kongamano Haki za Kidijitali na Ushirikishwaji wa 2023, ambalo hufanyika siku tatu kila mwakwa na kushirikisha wadau kadha kujadili sera za kijiditali barani afrika.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi huo, Mratibu mkuu wa Mtandao wa Cybersmart wa Afrika, David Moepeng alisema kuwa mtandao huo umeanzishwa kufuatia kufahamu kuwa, kadri Afrika inavyozidi kuwa ya kidijitali, watumiaji wa mtandao barani humo wanazidi kukabiliwa na aina mbalimbali za changamoto ya mtandao, hususan uhalifu wa kimtandao.
Kulingana na Moepeng, ambaye ni Mtaalamu wa Uhamasishaji wa Usalama wa Mtandaoni katika Cybersmart Botswana, uwezekano wa Waafrika kushambuliwa kwa mtandao unazidishwa na tabia na mazoea yanayozidi kuchipuka ya mtandao.
“Tabia hizi ni pamoja na kusambaza habari za kibinafsi na za siri kwenye mitandao ya kijamii, kujibu ujumbe wa ulaghai na aina nyingine za ulaghai mtandaoni, matumizi ya password yanayoweza kudukuliwa, na kuingia katika tovuti tofauti tofauti kwenye kompyuta na kujipata katika hatari ya kulaghaiwa.’’ Moepeng alidokeza.
Kwa hivyo Mtandao wa African Cybersmart umeundwa ili kuimarisha elimu kwa umma na kukuza tabia salama za mtandaoni kwa kuwezesha kujenga uwezo kupitia mafunzo, ushirikiano na kubadilishana maarifa kati ya wahamasishaji wa usalama wa mtandao pamoja na uhamasishaji wa rasilimali kwa kampeni za elimu kwa umma.
Katika Ripoti yake ya Afrika ya 2023 ya Tathmini ya Uhasama wa Mtandao, Interpol ilibainisha kuwa wahalifu wa mtandao hawakuzuiliwa na chochote kuweka watakalo mtandaoni, kwa kuwa hao hunawiri kwa njia hiyo katika biashara ya kuwalaghai watu.
Shirika la Kimataifa la Polisi wa Uhalifu lilishauri kwamba, kwa mantiki hiyo hiyo, jamii inafaa kushirikiana pamoja kwa kufahamishana na kupeana taarifa ili kudhibiti uhalifu mtandaoni.
“Ili kupunguza athari za uhalifu wa mtandaoni na kulinda jamii kwa ajili ya usalama wa ulimwengu, jamii lazima ifuate mienendo mipya na kubuni mbinu bunifu za kukabiliana nayo. Kufanya hivi kwa wakati ufaao kutakatisha njama na shughuli za uhalifu na vile vile kuwazua na mapema”, ilisema ripoti ya Interpol.
Kwa upande wake, Mratibu wa Afrika Mashariki wa Mtandao wa Cybersmart wa Afrika, Jackline Lidubwi, alisema uanachama katika mtandao huo upo wazi kwa mashirika yasiyo ya kutengeneza faida barani Afrika ambayo yanaendesha programu na kampeni za kuelimisha jamii kuhusu changamoto za mtandao.
Alibainisha kuwa, hali ya kawaida ya masaibu ya mtandao katika mipaka ya Afrika inahitaji mbinu sawa, hivyo basi uamuzi wa kuleta Afrika pamoja ni kukabiliana na changamoto ya mtandao kwa pamoja.
Lidubwi aliongeza kuwa mashirika wanachama yatafaidika na programu za mafunzo za mara kwa mara zinazokusudiwa kuhakikisha kuwa programu za elimu kwa umma katika bara hilo ziko sambamba na mienendo ya kisasa inayoibuk amtandaoni.