Uingereza yaondoa vizuizi vya usafiri kwa mataifa yote ya Afrika

Kufika leo Jumatano Uingereza itaziondoa nchi 11 za Afrika ikiwa ni pamoja na Afrika Kusini kutoka kwenye orodha inayozuia safari zinazoingia nchini humo, mawaziri walisema Jumanne.

Kufikia mwendo wa saa 0400 GMT siku ya Jumatano, mataifa yote yataondolewa kwenye orodha, alisema Katibu wa Uchukuzi Grant Shapps.

Serikali ya Uingereza ilichukua hatua ya kuyawekea vikwazo vya usafiri mataifa 10 ya Afrika Kusini ikiwemo Nigeria baada ya kugunduliwa kwa kirusi kipya cha Omicron. Kwa sasa, waingereza na raia wa Ireland pekee ndio wana haki ya kusafiri kutoka nchi zilizoorodheshwa na kuingia Uingereza, ila watabidi kukaa kwenye karantini wanapowasili nchini humo.

“Kama kawaida, tunazingatia hatua zetu zote za usafiri na tunaweza kuweka vizuizi vipya ikiwa kuna haja ya kufanya hivyo ili kulinda afya ya umma,” Shapps alitweet.

Waziri wa Afya Sajid Javid pia alitangaza hatua hiyo kwa wabunge bungeni huku Waziri Mkuu Boris Johnson akitafuta uungwaji mkono wa  vikwazo vyake vipya ili kupunguza kuenea kwa Omicron.

Mataifa yanayondolewa vizuizi ni:

  • Angola
  • Botswana
  • Eswatini
  • Lesotho
  • Malawi
  • Msumbiji
  • Namibia
  • Nigeria
  • Afrika Kusini
  • Zambia
  • Zimbabwe

Javid alisema marufuku ya kusafiri inaondolewa kwa kuwa “kwa sasa kuweka vizuizi vya usafiri hakusadii kudhibiti kuenea kwa kirusi cha Omicron kutoka mataifa ya nje.”