Ujerumani itaongeza msaada wake wa silaha kwa Ukraine kufuatia uvamizi wa Urusi kwa kutuma makombora 2,700 ya kutungulia ndege katika eneo la vita, chanzo cha serikali kiliiambia AFP siku ya Alhamisi.
Serikali ‘iliidhinisha uungwaji mkono zaidi kwa Ukraine ikitoa makombora ya kukinga ndege ya aina ya STRELA, ambayo hapo awali yalitumiwa na jeshi la Ujerumani Mashariki ya kikomunisti, chanzo hicho kilisema.
Shehena ya kwanza ya silaha za kivita 1,000 za Ujerumani na makombora mengine 500 ya kutungulia ndege tayari yametumwa Ukraine, serikali ilisema Jumatano.
Hatua hiyo imekuja baada ya Ujerumani kubadili sera yake ya muda mrefu ya kutopeleka silaha katika maeneo yenye migogoro, hali ambayo ina mizizi yake katika hatia ya vita vya enzi za Nazi nchini humo.
Siku ya Jumamosi, Kansela Olaf Scholz alitambua kwamba uvamizi wa Urusi ulidhihirisha ‘mabadiliko katika historia’ ambayo yalilazimisha Ujerumani kufikiria upya vipaumbele vyake.
Wakati huo huo, Ujerumani iliahidi kuwekeza euro bilioni 100 (dola bilioni 111) katika kuboresha vikosi vyake vya kijeshi mbele ya tishio la Urusi.
Siku ya Jumamosi serikali pia iliidhinisha kuwasilishwa kwa silaha zilizotengenezwa na Ujerumani kwa Ukraine kutoka nchi tatu, ikiwa ni pamoja na roketi 400 za vifaru zilizotumwa na Uholanzi.
Kabla ya kuongezeka kwa mzozo huo, Ujerumani ilikuwa imeahidi tu kuchangia kwa kutoa helmeti na kusaidia kujenga hospitali huko Ukraine.