Umoja wa Afrika siku ya Alhamisi ulilaani shambulizi la Urusi dhidi ya Ukraine na kutoa wito wa ‘kusitishwa mara moja kwa mapigano’ ukisema kuwa hali hiyo inaweza kuchangia kwa mzozo utakaoathiri dunia yote.
Mwenyekiti wa sasa wa muungano huo, Rais wa Senegal Macky Sall, na Moussa Faki Mahamat, mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, walisema katika taarifa yao ya pamoja ‘wana wasiwasi mkubwa’ na uvamizi huo.
Walitoa wito kwa Urusi ‘kuheshimu sheria za kimataifa na uhuru wa kitaifa wa Ukraine.’
Urusi ilizindua mashambulizi dhidi ya Ukraine siku ya Alhamisi, na kuua makumi ya watu huku mashambulio ya anga yakigonga vituo vya kijeshi na vikosi vya ardhini vikiingia kutoka kaskazini, kusini na mashariki.
Viongozi hao wa AU walisema kuwa mzozo kati ya mataifa hayo mawili unapaswa kutatuliwa kupitia ‘mazungumzo ya kisiasa’ yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa.
Kote Ukraine, takriban watu 68 waliuawa Alhamisi, wakiwemo wanajeshi na raia, kulingana na hesabu ya AFP kutoka vyanzo rasmi vya Ukraine.