Umoja wa Mataifa na mataifa kadhaa yametoa wito Alhamisi kusitisha vita vya Urusi nchini Ukraine, huku kukiwa hakuna uwezekano wa kufufua mazungumzo ya amani kati ya nchi hizo mbili.
“Uvamizi wa Urusi nchini Ukraine ni ukiukaji wa uadilifu wa ardhi yake na Mkataba wa Umoja wa Mataifa,” Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema alipokuwa katika mkutano wa Baraza la Usalama ulioandaliwa na Marekani.
“Lazima vita hivi vikome kwa ajili ya watu wa Ukraine, Urusi, na dunia nzima,” aliongeza.
Guterres hivi majuzi alizuru Moscow na Kyiv ili kutetea kuhamishwa kwa raia kutoka mji wa bandari wa Mariupol, ambapo mamia kadhaa ya watu wameweza kutoroka tangu wikendi.
Wajumbe wengi wa Baraza la Usalama, zikiwemo China, Marekani, Ireland, Ufaransa na Mexico walitoa wito wa kusitishwa kwa mzozo huo uliodumu kwa miezi kadhaa.
Balozi wa China katika Umoja wa Mataifa Zhang Jun alisisitiza kuwa ni diplomasia pekee ndiyo itamaliza mapigano hayo, akikosoa usafirishaji wa silaha kwenda Ukraine.
Mwenzake wa Kenya Martin Kimani alitoa wito wa upatanishi utakaosimamiwa na Guterres.
“Kila fursa lazima itumike kufikia amani,” balozi wa Ukraine katika Umoja wa Mataifa Sergiy Kyslytsya alisema.
Kulingana na wanadiplomasia, wanachama wasio wa kudumu wa Baraza la Usalama la Norway na Mexico waliwasilisha maoni yao yanayoonyesha “uungaji mkono mkubwa kwa juhudi za Katibu Mkuu na kutoa afisi zake nzuri katika kutafuta suluhu la amani.”
Kupitishwa kwa taarifa hiyo, ambayo itakuwa onyesho la kwanza la umoja katika baraza hilo tangu uvamizi wa Urusi Februari 24, bado hauna uhakika.
“Kuna wakati,” Naibu Balozi wa Urusi Dmitry Polyanskiy aliambia AFP alipoulizwa kama Moscow inaweza kuidhinisha makubaliano hayo.