Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini alionya siku ya Alhamisi kwamba karibu watu milioni tisa watahitaji msaada mwaka huu wakati nchi hiyo ikikabiliana na kuongezeka kwa ghasia kati ya makundi yenye silaha na mgogoro wa chakula.
Mapigano yamepamba moto upya katika taifa hilo changa zaidi duniani licha ya ahadi ya Rais Salva Kiir na mpinzani wake, Makamu wa Rais Riek Machar, kujitahidi kutekeleza vifungu muhimu vya mapatano ya amani ya 2018.
Nicholas Haysom, Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS), alitoa wito kwa viongozi hao kuongeza juhudi za kukomesha ghasia na kuitaka jumuiya ya kimataifa kuelekeza misaada zaidi nchini humo.
“Mwaka huu theluthi mbili ya watu au karibu watu milioni tisa — milioni 4.6 ambao ni watoto — watahitaji msaada wa dharura, Haysom aliwaambia waandishi wa habari katika mji mkuu wa Juba.
‘Ukosefu wa usalama wa chakula utaenea. Na kwa hiyo hali inazidi kuwa mbaya kwa sababu ya mabadiliko ya hali ya hewa, migogoro na watu kuyahama makazi yao.”
Haysom alisema “amesikitishwa na kuzuka upya kwa ghasia za kitaifa,” akiangazia masaibu ya maelfu ya watu waliofukuzwa kutoka makwao kutokana na mapigano yaliyozuka wiki iliyopita kati ya vikosi vinavyomuunga mkono Kiir na Machar katika Jimbo lenye utajiri mkubwa wa mafuta la Unity.
Mapigano hayo katika Kaunti ya Leer yalipelekea watu 14,000 kukimbia, kwa mujibu wa mamlaka za mitaa, huku Umoja wa Mataifa pia ukielezea wasiwasi kuhusu ripoti za unyanyasaji wa kingono, uporaji na uharibifu wa mali.
Kutoka jadi Leer imekuwa ngome inayomuunga mkono Machar, ilikuwa kitovu cha mzozo wa kibinadamu ambao uliibuka kutoka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya 2013-2018.
Sudan Kusini imekumbwa na mizozo tangu uhuru mwaka 2011 huku vita vikigharimu maisha ya karibu watu 400,000.
Haysom alisema kuongezeka kwa mapigano kunaongeza idadi ya watu wanaohitaji msaada na kuongeza masaibu kwa watu kutokana na mafuriko yanayotarajiwa katika maeneo mengi katika miezi ijayo.
Ufadhili unaoendelea na wa kutosha unahitajika haraka ili kukomesha madhara mabaya zaidi kutokea.
Kiir na Machar mapema mwezi huu walikubaliana juu ya kuundwa kwa amri ya pamoja ya vikosi vya kijeshi — sehemu muhimu ya mkataba wa amani — na Haysom alisema anatumai itafungua mazungumzo ya kushughulikia matatizo ambayo nchi inakabiliana nayo.
“Huku ikiwa imesalia miezi 10 katika kipindi cha mpito, sasa ninahimiza pande zote kuelekeza nguvu mpya katika kukamilisha vigezo vilivyosalia vya makubaliano ya amani na kufikia mwafaka kuhusu ni lini uchaguzi unapaswa kufanywa,” Haysom alisema.