Umoja wa Mataifa ulisema Jumanne kuwa umetoa wito wa dharura kusaidia mamia kwa maelfu ya watu katika maeneo ya Afghanistan yaliyokumbwa na tetemeko la ardhi lililosababisha vifo wiki jana.
Tetemeko hilo la kipimo cha 5.9 katika kipimo cha Richter Jumatano iliyopita lilipiga pakubwa zaidi jimbo maskini la Paktika mashariki mwa nchi, na kuua zaidi ya watu 1,000 na kuwaacha makumi kwa maelfu bila makazi.
Shirika la Umoja wa Mataifa la kutoa misaada ya kibinadamu lilisema kuwa shirika hilo na washirika wake wametoa ombi la dola milioni 110 kusaidia haraka watu 362,000 kwa muda wa miezi mitatu ijayo katika maeneo yaliyoathirika zaidi ya majimbo ya Paktika na Khost.
“Mbali na vifo na majeruhi, tetemeko hilo pia liliharibu nyumba, vituo vya afya, shule na mitandao ya maji, na kuacha maelfu ya watu wakiwa katika hatari ya kuathirika zaidi,”msemaji Jens Laerke aliwaambia waandishi wa habari.
Alisema ombi la msaada iliyozinduliwa Jumatatu ni sehemu ya Mpango wa jumla wa Mwitikio wa Kibinadamu wa mwaka huu kwa nchi hiyo masikini na yenye migogoro.
Ili kutekelezwa kikamilifu, hiyo itahitaji dola bilioni 4.4, lakini hadi sasa imefadhiliwa kwa asilimia 34 tu, Laerke alisema.
Kwa hakika, alisema, mpango wa Umoja wa Mataifa haufadhiliwi kwa kiasi kikubwa kwani wakala na washirika wake wamelazimika kukopa vifaa na wafanyakazi kutoka kwa programu nyingine za kibinadamu ili kusaidia kukabiliana na tetemeko la ardhi mara moja.
Ijumaa iliyopita, mkuu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu Martin Griffiths pia alitoa dola milioni 10 kutoka UN Central Emergency Relief Fund kusaidia kuongeza msaada huo.