Upasuaji Wa Mwili Wa Mwanablogu Albert Ojwang Kuendelea Leo Katika Hifadhi Ya Maiti, Jijini Nairobi

Zoezi la Upasuaji wa mwili wa mwanablogu Albert Ojwang unafanyika leo katika Hifadhi ya Maiti ya Nairobi baada ya kuahirishwa hapo awali.

Upasuaji Wa Mwili Wa Mwanablogu Albert Ojwang Kuendelea Leo Katika Hifadhi Ya Maiti, Jijini Nairobi

Mwanapatholojia Mkuu wa Serikali nchini Kenya, Dkt. Johansen Oduor, alijiondoa kwenye uchunguzi huo kutokana na mgongano wa maslahi, akisema ana uhusiano wa kifamilia na marehemu.

Familia ya Ojwang pamoja na wanaharakati wa haki za binadamu wamekuwa wakishinikiza uchunguzi huru, wakidai kuwa mazingira ya kifo chake akiwa mikononi mwa polisi ni ya kutatanisha.

Albert Ojwang alikamatwa mnamo Jumamosi, Juni 7, 2025, kufuatia malalamishi kutoka kwa Naibu Inspekta wa polisi aliyemshutumu kwa kumharibia jina kupitia mitandao ya kijamii.

Inadaiwa kuwa Ojwang alikuwa ameandika chapisho kwenye ukurasa wake wa X (zamani Twitter) akimtuhumu afisa huyo kwa kushiriki katika vitendo vya ufisadi.

Polisi walifika nyumbani kwake katika kijiji cha Kakoth, Kaunti ya Homa Bay, na kumtia mbaroni bila kutoa maelezo ya kina kwa familia yake.

Baada ya kukamatwa, alisafirishwa hadi Kituo cha Polisi cha Central jijini Nairobi, jambo ambalo lilizua mjadala mkali huku familia yake ikidai kuwa haikujulishwa kuhusu safari hiyo  simu yake ilizimwa.

Siku ya Jumatatu, 9 Juni, 2025, Inspekta mkuu wa polisi nchini Kenya, Douglas Kanja alithibitisha kuwa mwanablogu huyo alizuiliwa rasmi katika Kituo Kikuu cha Polisi chini ya OB nambari 136/7/6/2025.
Kanja alisema kuwa Ojwang alikamatwa kufuatia malalamishi yaliyowasilishwa na Naibu Inspekta Jenerali Eliud Lagat, ambaye alimshtumu kwa kumharibia jina.

Baada ya kukamatwa, Ojwang alihojiwa Jumamosi kabla ya kuhamishwa hadi kitengo cha kuzuilia ndani ya kituo hicho.
Hata hivyo, kulingana na ripoti, polisi baadaye walimpata akiwa amepoteza fahamu katika seli yake na kumkimbiza katika Hospitali ya Mbagathi, ambapo alitangazwa kuwa amefariki alipofika.

Hali hiyo imezua hisia kali miongoni mwa Wakenya, huku wengi wakitaka uwajibikaji na uchunguzi wa kina kuhusu sababu halisi ya kukamatwa kwake na mazingira ya kifo chake.

Baada ya kukamatwa, Ojwang alizuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Central, Nairobi, ambako alifariki saa chache baadaye katika mazingira yanayotiliwa shaka

Ripoti za awali kutoka kwa Polisi zilidai kuwa Ojwang alipatikana akiwa amepoteza fahamu ndani ya seli ya Kituo cha Polisi cha Central, wakidai huenda lilikuwa jaribio la kujiua.

Hali ya usalama imeimarishwa nje na ndani ya makafani, huku waandamanaji wakitaka uwajibikaji na haki kwa marehemu.

Uchunguzi huu unatarajiwa kutoa mwanga kuhusu chanzo cha kifo chake na iwapo kulikuwa na ukiukaji wa haki za binadamu.