Viongozi wa upinzani nchini Uganda siku ya Jumanne walikashifu uamuzi wa serikali wa kuwanunulia maofisa waandamizi wa bunge gari la kifahari aina ya Limousine huku mfumuko wa bei nchini humo ukipanda.
Nchi ya watu milioni 45 imeathiriwa sana na janga la UVIKO 19 na vita nchini Ukraine, huku bei ya vyakula ikipanda katika wiki za hivi karibuni huku Rais Yoweri Museveni akipuuza wito wa kupunguzwa kwa ushuru na ruzuku,badala yake akiwataka raia kupunguza matumizi yao.
Ununuzi wa shilingi bilioni 2.4 (dola 640,000) wa gari mbili za limousine kwa spika wa bunge na naibu wake umechochea hasira ya umma, huku kiongozi mkuu wa upinzani nchini humo, Bobi Wine, akiishambulia serikali kwa kushindwa ‘kutanguliza maisha magumu ya Waganda.”
“Tutatumiaje bilioni 2.4 kununua magari mawili kwa spika na naibu spika kuhudhuria sherehe wakati mamilioni ya Waganda wanalala njaa, wakati watu hawawezi kumudu misingi ya maisha,” rapper huyo aliyegeuka kuwa mwanasiasa aliiambia AFP.
Mpinzani wa Museveni na aliyekuwa mgombea urais Kizza Besigye, ambaye ameshtakiwa kwa kuchochea ghasia baada ya kuwataka Waganda kuandamana kupinga kupanda kwa bei, aliita ununuzi huo “kashfa.”
“Ni wazi kuwa hii ni serikali ya vimelea na inabidi ikomeshwe,”
Lakini kamishna wa bunge la Uganda, Prossy Akampurira Mbabazi, siku ya Jumanne alitetea uamuzi wa kununua magari hayo. “Hasira za umma hazifai.”
“Magari ambayo spika na naibu walikuwa wakitumia yalikuwa na umri wa miaka 10 na ilibidi yabadilishwe,” alisema.
Katika hotuba yake ya kila mwaka ya hali ya taifa siku ya Jumanne, Museveni alisema kuwa ‘kukatwa kwa ushuru na ruzuku, haswa kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje, ni kujiua kwa sababu watu wetu wanaweza kununua ovyo na mwishowe tunamaliza akiba yetu ya fedha za kigeni.”
Julius Mukunda, mkurugenzi mtendaji wa Asasi ya Kiraia ya Civil Society Budget Advocacy Group cha mashirika ya kiraia, aliiambia AFP “ununuzi huo ulikuwa mbaya na tofauti na wito wa rais kwa watu kupunguza ununuzi wao.”