Urusi siku ya Alhamisi ilipiga marufuku ya kusafiri kwa Makamu wa Rais wa Amerika Kamala Harris, mkuu wa Facebook Mark Zuckerberg na makumi ya Wamarekani mashuhuri na Wacanada kulipiza kisasi kwa vikwazo vilivyowekwa juu ya uvamazi wao nchini Ukraine.
Wizara ya mambo ya nje ya Urusi ilisema vizuizi vya kusafiri kwa Wamarekani 29 na Wacanada 61 — ambavyo pia vinajumuisha maafisa wa ulinzi, viongozi wa biashara na waandishi wa habari kutoka nchi zote mbili – vitaendelea kutumika kwa muda usiojulikana.
Mjini Washington, mmoja wa maafisa waliolengwa, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Ned Price, alisema kwamba marufuku ya kusafiri ni heshima kwake.
Amerika imeongoza juhudi za kimataifa za kuiwekea Urusi vikwazo vikali kutokana na operesheni yake ya kijeshi nchini Ukraine na kusababisha msukosuko katika uchumi wake.
Amerika na Umoja wa Ulaya zimewawekea vikwazo Warusi kadhaa akiwemo Rais Vladimir Putin, binti zake na matajiri wanaoonekana kuwa muhimu kwa mamlaka ya kiongozi huyo wa Urusi.
Waamerika wengine waliopigwa marufuku Alhamisi na Urusi ni pamoja na mtangazaji wa televisheni ya ABC News George Stephanopoulos, mwandishi wa gazeti la Washington Post David Ignatius na mhariri wa tovuti ya habari ya Meduza anayeangazia Urusi Kevin Rothrock.
Maafisa hao wa ulinzi wa Marekani ni pamoja na msemaji wa Pentagon John Kirby na Naibu Waziri wa Ulinzi Kathleen Hicks.
Orodha ya Wacanada waliopigwa marurfuku inaongozwa na Cameron Ahmad, ambaye anahudumu kama mkurugenzi wa mawasiliano kwa Waziri Mkuu Justin Trudeau, na Kamanda wa Kikosi Maalum cha Operesheni cha Kanada Steve Boivin.
Awali Urusi ilikuwa imepiga marufuku Facebook na Instagram, ambazo ni sehemu ya himaya ya Zuckerberg ya Meta, ikiziita mashirika ya itikadi kali.