Kikosi cha kijeshi cha Mali kilisema Jumatatu kilizuia jaribio la mapinduzi wiki iliyopita lililoongozwa na maafisa wa jeshi na kuungwa mkono na nchi ya Magharibi ambayo haikutajwa jina.
Taarifa hiyo iliyosomwa kwenye televisheni ya serikali ilisema “kundi dogo la maafisa wa Mali walijaribu kufanya mapinduzi usiku wa Mei 11 hadi 12, 2022.”
“Askari hawa waliungwa mkono na serikali ya Magharibi. Jaribio hilo lilizimwa kutokana na umakini na weledi wa vikosi vya ulinzi na usalama.”
Taarifa hiyo ilitoa maelezo machache juu ya kile kinachodaiwa kutokea.
Ilitaja waliokamatwa na kusema wafungwa hao watafikishwa mahakamani.
Utambulisho wao na mahali walipo haukufichuliwa.
Iliongeza kuwa usalama umeimarishwa karibu na mji mkuu Bamako na katika mipaka na Mali.
Chanzo cha kijeshi kilichozungumza kwa sharti la kutotajwa jina kilizungumza kuhusu kukamatwa kwa watu 10 na kusema wengine walikuwa wangali wanasakwa.
Taarifa ya serikali ilisema inatumia njia zote ili kuwapata washiriki wa jaribio hilo la mapinduzi.
Hakuna dalili yoyote ya jaribio la mapinduzi lililoripotiwa hadi Jumatatu jioni.
Mali imepitia mapinduzi mawili ya kijeshi tangu Agosti 2020, wakati jeshi lilipompindua rais aliyechaguliwa Ibrahim Boubacar Keita.
Taifa hilo la Afrika Magharibi limekuwa likipambana na waasi wa kijihadi dhidi ya makundi yenye mafungamano na Al-Qaeda na kundi la Islamic State tangu mwaka 2012 kaskazini na katikati mwa nchi.
Mapigano hayo pia yameenea hadi nchi jirani za Niger na Burkina Faso.
Serikali ya nchi hiyo inayotawaliwa na jeshi imevunja uhusiano na mshirika wa jadi Ufaransa na kuanzisha uhusiano wa karibu na Urusi katika vita vyake dhidi ya wanajihadi.
Ilikuwa imeahidi kurudisha mamlaka kwa raia ifikapo Februari 2022 lakini tangu wakati huo imeongeza muda wa kurudishwa kwa uongozi wa katiba, na kusababisha vikwazo vya kikanda.