Maandamano yaliyoitishwa na jeshi tawala nchini Mali kupinga vikwazo vikali vya kikanda yalitarajiwa kuanza Ijumaa huku shinikizo la kimataifa likiongezeka kuhusu kucheleweshwa kwa uchaguzi.
Viongozi kutoka jumuiya ya Afrika Magharibi ECOWAS walikubali kuiwekea vikwazo Mali wiki jana, na kuweka vikwazo vya kibiashara na kufunga mipaka, katika uamuzi ulioungwa mkono baadaye na Ufaransa, Amerika na Umoja wa Ulaya.
Hatua hiyo ilifuatia pendekezo la serikali ya Mali ya kusalia madarakani kwa hadi miaka mitano kabla ya kuandaa uchaguzi — licha ya matakwa ya kimataifa kwamba iheshimu ahadi ya kufanya uchaguzi mwezi Februari.
Wanajeshi hao walitaja vikwazo hivyo kama “vilivyokithiri” na “vya kinyama” na wakataka maandamano yafanyike.
Kanali Assimi Goita, aliyechukua uongozi katika mapinduzi ya mwezi Agosti 2020, pia amewataka Wamali “kutetea nchi yao”.
Katika mji mkuu Bamako, maandamano yalipaswa kuanza karibu saa sita mchana, ikifuatiwa na sala na mfululizo wa hotuba.
Waziri mkuu wa mpito wa Mali Choguel Kokalla Maiga alitarajiwa kuongea mwendo wa saa 1700 GMT.
Pamoja na kufunga mipaka na kuweka vikwazo vya kibiashara, viongozi kutoka Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) pia walisitisha msaada wa kifedha kwa Mali na kuzuia fedha za nchi hiyo katika Benki Kuu ya Mataifa ya Afrika Magharibi.
Vikwazo hivyo vinatishia kuharibu uchumi ambao tayari unayumbayumba. Mali ni mojawapo ya nchi maskini zaidi duniani.
Uasi wa kikatili wa wanajihadi pia umeendelea nchini Mali tangu mwaka 2012, huku maeneo mengi ya eneo la nchi hiyo yakiwa nje ya udhibiti wa serikali.
Mashirika kadhaa ya ndege, ikiwa ni pamoja na Air France, yamesitisha safari za ndege kwenda Bamako.
Mali pia iko katika hatari ya uhaba wa pesa. Kako Nubukpo, kamishna katika Muungano wa Kiuchumi na Fedha wa Afŕika Maghaŕibi, alisema kuwa “Mali imetengwa na mataifa mengine duniani.”
Ufaransa, mkoloni wa zamani wa Mali, na Amerika zote zimeeleza kuunga mkono vikwazo vya ECOWAS.
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrel alisema siku ya Alhamisi kwamba Brussels itafuata ECOWAS katika kuchukua hatua dhidi ya Mali kutokana na kucheleweshwa kwa uchaguzi.
Siku hiyo hiyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema “ni muhimu sana kwa kwamba serikali ya Mali iwasilishe ratiba ya uchaguzi inayokubalika.”
Licha ya shinikizo hilo, wengi nchini Mali wameunga mkono jeshi, huku jumbe za utaifa zikimiminika kwenye mitandao ya kijamii.
Uhusiano wa Mali na majirani na washirika wake umezidi kuzorota tangu mapinduzi yaliyoongozwa na Goita Agosti 2020 dhidi ya rais Ibrahim Boubacar Keita.
Chini ya tishio la kuwekewa vikwazo, Goita aliahidi kuandaa uchaguzi wa rais na wabunge, na kurejesha utawala wa kiraia ifikapo Februari 2022.
Lakini alifanya mapinduzi ya pili mnamo Mei 2021, na kuiondoa serikali ya muda ya kiraia na kuvuruga ratiba ya kurejesha uongozi wa demokrasia.
Goita pia alijitangaza kuwa rais wa muda.
Serikali yake imesema kuwa ukosefu wa usalama uliokithiri nchini Mali unaizuia kuandaa uchaguzi mwishoni mwa Februari.