Uuzaji wa tikiti za Kombe la Dunia litakalofanyika Qatar ulizinduliwa kwa bei ya chini Jumatano huku wakaazi na watu waliohamia nchini humo wakipata nafasi ya kuhudhuria dimba hilo kwa kulipa kiasi cha $ 11 tu huku wasiwasi ukiendelea kuwepo juu ya UVIKO-19.
Mamlaka bado haijatangaza ni mashabiki wangapi wataruhusiwa kuingia viwanjani kwa ajili ya Fainali za kwanza za Kombe la Dunia kuwahi kufanyika katika nchi ya Kiarabu. Dimba la Kombe la Dunia litaanza Novemba 21 hadi Desemba 18.
Shirikisho la soka duniani FIFA lilifungua droo ambayo inatoa tikiti za mechi kwa mtu binafsi kwa dola 69 tu kwa mashabiki wa kimataifa — karibu theluthi moja chini ya kiwango walichotozwa mashabiki wa kimataifa katika michuano kama hiyo iliyofanyika Urusi 2018 — lakini tikiti ya fainali inaweza kugharimu hadi $1,607.
Wakaazi wa Qatar, wakiwemo wafanyakazi waliohamia nchini humo wataweza kupata tikiti kwa chini ya $11.